NEWS

Monday 5 July 2021

Wamiliki walalamikia notisi ya kutaka kubomolewa nyumba Tarime, wakusudia kuweka zuio




WAMILIKI wa nyumba zilizopo kandokando mwa barabara ya Tarime Mjini – Nyamwaga, wamekutana kuweka mpango wa kupinga notisi ya siku 30 ya kuwataka wabomoe nyumba hizo.

Wakizungumza katika kikao chao kilichoongozwa na Mwenyekiti wao, David Mroni mjini Tarime juzi, wamiliki hao ambao nyumba zao zimewekewa alama X, wamedai kuwa kitendo hicho ni cha uonevu, kwani nyumba hizo zina hati miliki na Halmashauri ya Mji wa Tarime imekuwa ikikusanya kodi.

Wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea barua iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Tarime, Erasto Mbunga ya Juni 30, 2021 ikieleza kuwa agizo hilo limetolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kupisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Barua hiyo inawataka kubomoa nyumba zilizo ndani ya hifadhi ya barabara hiyo ndani ya siku 30, la sivyo TANROADS itazibomoa kwa gharama za wenye nyumba.



Wamiliki hao wanalalamikia hatua hiyo wakisema itawaathiri kiuchumi na wengi wao ni wazee wanaotegemea nyumba hizo kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao na familia zao.

Katika mkutano huo, wamemshirikisha Wakili Otieno Onyango kwa ajili ya ushauri na msaada wa kisheria ili kuzuia mpango wa kubomolewa nyumba zao.

Wamesema haiwezekani nyumba walizojenga kwa kuzingatia bikoni zilizowekwa na wataalamu wa ardhi, wakapewa hati miliki na kuzilipia kodi serikalini kwa miaka mingi, leo zionekane ziko ndani ya hifadhi ya barabara na kutakiwa kubomolewa.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages