NEWS

Tuesday 27 July 2021

Wananchi Tarime Vijijini walia ukosefu wa huduma za kijamii


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Apoo Castro Tindwa.

WAKAZI wa kijiji cha Kitawasi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), wameiomba Serikali kuwatatulia kero zinazowakabili, zikiwemo za ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa maji safi na salama, umeme na kituo cha huduma za afya.

Wananchi hao wamesema hali hiyo inakifanya kijiji hicho kuwa kama kisiwa, kwa kukosa huduma muhimu za kijamii, ambapo inadaiwa baadhi ya wajawazito na wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma za matibabu za uhakika na kwa wakati.

Wakizungumza na Mara Online News kwa njia ya simu hivi karibuni, wanakijiji hao wamesema wanakabiliwa na changamoto hizo tangu nchi ipate uhuru, mwaka 1961.

Kutokana na ukosefu wa zanahati kijijini, wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilomita 28 kwenda kutafuta huduma za afya kaika kata jirani ya Muriba, huku wagonjwa na wajawazito wakibebwa kwenye baiskeli.

“Tuna shida sana maana barabara ni mbovu, haipitiki kwa gari, na eneo hilo [Muriba] ni vigumu kufika kutokana na kuwa na milima mikubwa,” alilalamika Wankyo Karebu.

“Baadhi ya akinamama wajawazito wamekuwa wakijifungulia njiani na wengine wamekuwa wakipoteza maisha pamoja na watoto wao kutokana na umbali uliopo kutoka kijiji cha Kitawasi hadi Muriba, kwani wamekuwa wakikosa huduma ya wakunga, wauguzi na waganga wa kuwahudumia kwa wakati,” amesema Edward Nyagana.

“Yaani sisi huku tuna sida sana, wazazi wangu wakati nikiwa mtoto mdogo waliniambia barabara hiyo ilikuwa inapitika miaka ya 50’, lakini kwa sasa haipitiki,” amesema John Nyabanke (60) na kuungwa mkono na Mwita Mohono, wote wakazi wa Kitawasi.

Wananchi hao wameiomba Serikali kusikiliza kilio chao kwa kufungua barabara kutokea Shule ya Msingi Kitawasi, kupitia Kanisa la Wasabato, vitongoji vya Kitawasi, Lemerera, Nyarukoba, Makabano kuelekea Bung’eng’e na Genkuru.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kitawasi, Robi Mageji na Diwani wa Kata ya Gorong’a, Ayub Marwa, wamekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kwamba Serikali inajipanga kuzitafutia ufumbuzi.

Hata hivyo, Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwatafuta viongozi wa ngazi ya wilaya hiyo, ili kujua kama kuna hatua zozote zinachukuliwa kutatua kero za wanakijiji hao.

(Imeandikwa na Ahmed Makongo wa Mara Online News)

1 comment:

  1. Mm inanuma Sana unatakuta mubuge yupo na kila siku anaenda bugeni hachangii hoja yoyote kazi kupinga makofi tu wanachi wanateseka

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages