NEWS

Wednesday 28 July 2021

Wananchi walalamikia kero ya mabonde, ukosefu wa taa stendi ya MusomaHali halisi ya stendi ya mabasi Bweri, Musoma kipindi cha msimu wa mvua.

UBOVU wa stendi ya mabasi ya mkoa wa Mara, iliyopo eneo la Bweri katika Manispaa ya Musoma, umeendelea kuzua minong’ono na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wakihoji ukimya wa viongozi kuhusu kero hiyo ya muda mrefu sasa.

Ujenzi wa stendi hiyo ulianza kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, baada ya Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete kuuwekea jiwe la msingi, mwaka 2010.

Taarifa zilizopo ni kwamba stendi hiyo imejengwa chini ya kiwango cha ubora kilichokusudiwa, licha ya kugharimu mamilioni ya fedha za walipakodi, huku mkandarasi anayedaiwa kuboronga ujenzi huo akishindwa kurekebisha mapungufu na kuukamilisha.

“Yaani baada ya agizo la Rais wa Awamu ya Tano kuwa mradi wa stendi hii ukamilike, tulitembelea eneo la mradi na kukuta kazi iliyofanywa na mkandarasi ni chini ya viwango na hata pesa iliyobaki hakuna kitu kitakachofanyika,” chanzo chetu cha habari kutoka serikalini mkoani Mara kimeiambia Mara Online News, juzi.

Wananchi wa Manispaa ya Musoma wanaelezea kushangazwa kwao na ukimya wa viongozi waliopewa agizo la kufuatilia na kusimamia ili kuhakikisha ujenzi wa stendi hiyo unakamilishwa kwa ubora unaotakiwa.

Inadaiwa kuwa shilingi milioni 600 zilikuwa zimetengwa na serikali miezi kadhaa iliyopita, kwa ajili ya kukamilisha mradi huo wa stendi ya mabasi.

“Mheshimiwa Rais aliyetangulia mbele za haki [Hayati Dkt John Pombe Magufuli] alipofika hapa [Musoma] aliagiza kwamba uboreshaji wa stendi hii ukamilishwe ndani ya siku tano, lakini tulishangaa baada ya muda waliweka kifusi tu wakatoweka,” Daniel John ambaye ni mwendesha bodaboda anayeegesha katika stendi hiyo, ameiambia Mara Online News.

John amesema ubovu wa stendi ya mabasi Bweri unasababisha adha kubwa kwa bodaboda na wajasiriamali, wakiwemo wanawake wanaojishughulisha na biashara ndogondogo kujitafutia riziki katika stendi hiyo.

“Mvua ikinyesha stendi inajaa maji, kuna kasoko kako hapo pembeni [mwa stendi hiyo], ambako pia mvua ikinyesha inakuwa kero kwa akina mama lishe,” John ameongeza.

Naye Yohana Jumanne ambaye ni machinga, amekiri kuwa stendi hiyo imegeuka kuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara na abiria.

“Hii stendi hata haina hadhi ya kuitwa stendi ya mkoa, mvua ikinyesha maji yanatwama, yanajaa stendi na tunakosa sehemu ya kupita,” Jumanne amesema.

Katibu wa stendi hiyo, Yusufu Mwambara ameiambia Mara Online News kwamba kero nyingine ni pamoja na jengo la abiria na vibanda vya maduka kutokidhi viwango, vyoo kuwa mbali na stendi - huku navyo vikiwa vibovu na ukosefu wa taa, hali inayohatarisha usalama nyakati za usiku.

Mwambara ametaja matatizo mengine kuwa ni ukosefu wa huduma ya maji, bodaboda na taxi kutotengewa maeneo ya kuegesha, huku wafanyabiashara ndogondogo wakizagaa kila mahali.

Mara Online News imedokezwa kuwa viongozi wa wilaya ya Musoma baada ya agizo la Rais wa Awamu ya Tano, walitembelea stendi hiyo lakini hawakufikia uamuzi kuhusu uboreshaji wa mradi huo.

“Unajua viongozi walipotembelea ile stendi walikuta hata nyumba zilizojengwa na mkandarasi zimeanza kubomoka, yaani sasa ikawa changamoto,” kimesema chanzo chetu cha habari.

Kutokana na kero hizo kudumu muda mrefu, wananchi wa Manispaa ya Musoma waliozungumza na Mara Online News, wametumia nafasi hiyo kumwomba Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Ally Salum Hapi na Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati, ili stendi hiyo iboreshwe na kuwaondolea watumiaji usumbufu.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kutafuta mamlaka husika ziweze kuzungumzia sababu za kuchelewa kwa uboreshaji wa stendi hiyo, kinyume cha agizo la kiongozi wa nchi.

(Imeandikwa na Mara Online News, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages