NEWS

Wednesday 28 July 2021

Wawekezaji walalamikia ukiritimba, utapeli huduma za LATRA



MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) Mkoa wa Mara, imelalamikiwa kwa ukiritimba katika utoaji huduma za vibali na leseni kwa wawekezaji.

Wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti mkoani Mara hivi karibuni, baadhi ya wananchi wenye kampuni za uwekezaji wamelalamika kuwa LATRA mkoani humo imekuwa ikiwapiga ‘danadana’ na kudai tozo nyingi zisizo na maelezo wanapohitaji leseni za kuendeshea kampuni zao.

“Mwanzoni niliwasiliana na ofisa wa LATRA Mkoa wa Mara kwa ajili ya kupata leseni ya gari la kampuni yangu, akanitaka nilipe shilingi lakini moja - nikalipa, kisha akanielekeza nikaenda Polisi kulipia gharama nyingine, baada ya hapo akaniambia kuna mtu atanitumia ‘control number’ kwa ajili ya huduma hiyo.

“Cha ajabu mtu ambaye niliambiwa atanitumia ‘control number’, alinitumia kupitia namba tofauti ya simu na kutaka nilipe shilingi 255,000 bila maelezo yoyote,” Mseti Nyaronyo ambaye ni Mkurugenzi wa Goldland Hotel & Tours, ameiambia Mara Online News.

Pia yapo malalamiko mengine kwamba kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na watu wanaojitambulisha kama mawakala wa LATRA na kutapeli wananchi wanaohitaji huduma za mamlaka hiyo, kwa kuwaomba fedha ili wawahudumie bila mafanikio.

Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu juzi, mtumishi wa LATRA, Daudi Sagara aliyejitambulishwa kuwa ni Afisa Leseni, amekiri kuwepo kwa maombi ya leseni kutoka kwa Nyaronyo, lakini amekana mamlaka hiyo kuwa na wakala yeyote wa kuiunganisha na wateja wao.

“Huyo Nyaronyo wa Goldland tuliwasiliana naye nikamwambia akalipia shilingi laki moja ili mfumo umruhusu kuendelea na maombi ya leseni ya gari.

“Kimsingi mteja anapaswa kufanya hivyo mwenyewe kwa njia ya mfumo, lakini changamoto iliyopo ni kwamba kuna wateja wasiojua kutumia mfumo, kwa hiyo wanatafuta msaada wa kufanyiwa maombi na kupata ‘control number’.

“Sisi maelewano yao huwa hatuyajui, iliwahi kuvuma kipindi fulani tukapiga marufuku vishoka (matapeli), wenyewe huko wanawaita mawakala, japokuwa sisi hatuna wakala huko. Kwa hiyo, ‘control number’ huwa inatoka huko huko kwenye mfumo, mteja analipa mwenyewe,” Sagara ameeleza na kuahidi kuchukua hatua za kuepusha utapeli kwa wateja wa LATRA.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages