NEWS

Thursday, 25 December 2025

Waziri Nyansaho afikisha salamu za Rais Samia kwa wazee wa Mara


Waziri Dkt Nyansaho (watatu kulia) na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wazee wa mkoa wa  Mara jana.


Na Mwandishi Wetu, Mara

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Rhimo Nyansaho, amekutana na wazee wa wilaya zote za mkoa wa Mara kuzungumzia, pamoja na mambo umengine, umuhimu wa taifa kulinda amani yake.

“Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aliona mliyokuwa mnahimiza amani na kukemea uvunjifu wake, na amenituma niwafikishie salamu zake na kuwashukuru kwa kulinda amani hiyo,”Dkt Nyansaho aliwaambia wazee hao katika kikao kilichofanyika wilayani Tarime jana.Aliwaomba wazee wa mkoa huo kuendelea kuimarisha na kuhimiza uwepo wa tunu ya amani kwa maendeleo ya mkoa huo na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt Rhimo Nyansaho, akisisitiza jambo katika kikao hicho.


“Huwezi kufanya maendeleo yoyote kama hakuna amani. Amani ni chanzo cha maendeleo kwa kila sehemu,” alisema waziri mzaliwa wa mkoa wa Mara katika wilaya ya Serengeti.
Alisema mkoa wa Mara una historia kubwa na kusisitiza kuwa unapaswa kuwa mfano kwa kila jambo ikiwa ni sehemu ya kumuenzi mwasisi Taifa la Tanzania hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere.

Alihawakikishia wazee hao kuwa serikali awamu ya sita chini itaendelea kujali kundi la wazee huku akitolea mfano wa utoaji wa bima ya afya kwa ajili ya matibabu yao.
“Bima ya afya kwa wazee ni sehemu ya kipaumbele na utekezelezaji wake upo katika zile siku 100 za uongozi wa wa Rais Samia,” Dkt Nyansaho alisema.

Wazee wa mkoa wa Mara wakimsikiliza Waziri Dkt Nyansaho katika kikao hicho.


Pia alisema ataendelea kushirkiana na wabunge wa majimbo wa mkoa wa Mara ili kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya mkoa huo ambayo ipo katika ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa reli ya Tanga-Arusha- Musoma na ujenzi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Serengeti.

“Nitajitahidi kushirikiana na wenzangu ( akimaanisha wabunge wa mkoa wa Mara) ili 2030 tuwe tumefikia pazuri,” alisema Dkt Nyansaho, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na JKT pia aliteuliwa kuwa Mbunge wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Dkt Samia.
Mkuu wa Mkoa wa Mara akizungumza katika kikao hicho.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alisema hali ya mkoa huo kiusalama ni shwari, huku akiwatakia wananchi wote heri ya Krismasi . Kanali Mtambi aliwashukuru wazee hao na kusisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kudumisha na kulinda amani.

“Tuendelee kuhakikisha amani inatamalaki, jukumu la kulinda amani ni letu sote,“ alisema kwenye kikao hicho ambacho pia kiluhudhuriwa na Mwenyekti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Fadhli Maganya, mtoto wa Baba wa Taifa , Madaraka Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Matera Chacha Newland.
Kwa upande wake, mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa, Mzee Christopher Mwita Gachuma, ambaye alikuwa mwenyeji wa kikao hicho, alimwelezea Dkt Nyansaho kama kiongozi kijana mwenye maono ambaye amekuwa akiacha alama kila eneo ambalo analisimamia.

“Dkt Nyansaho ni kijana anayependa maendeleo, anaacha alama kila mahali,” alisema Gachuma, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Mara (NEC). Kabla ya kuteuliwa kuwa Mbunge na Waziri, Dkt Nyansaho alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF.

Wazee wa mkoa huo walimshukuru Rais Samia kwa kumwani Dkt Nyansaho na kumteua kuwa Mbunge na kisha kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kuahidi kuipatia serikali ushirikiano katika kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu .

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages