NEWS

Thursday 19 August 2021

ATFGM Masanga hakuna kulala mapambano dhidi ya ukeketaji maeneo ya mpakani
WADAU wa mapambano dhidi ya ukeketaji kutoka maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Kenya, wamesisitiza umuhimu wa viongozi wa kijamii, serikali, dini na asasi za kiraia kuongeza ushirikiano katika juhudi za kukomesha tatizo hilo.

Wakizungumza katika mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Shirika la ATFGM Masanga mjini Tarime, Tanzania leo Agosti 19, 2021, wadau hao wameongeza kuwa mikakati ya kudhibiti ukeketaji ihusishe pia suala la kuelimisha jamii nzima athari za vitendo hivyo.

“Tuelimishe jamii madhara ya ukeketaji, lakini pia tuongeze nguvu ya kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ngariba (wakeketaji), waandaaji na washiriki wote wa sherehe za ukeketaji,” amesema Kamishna Msaidizi wa Kaunti ya Migori nchini Kenya, Kelvin Mwasambu.


Washiriki mkutanoni

Akizungumzia mapambano dhidi ya ukeketaji nchini Kenya, Meneja Mipango wa Bodi ya Kupinga Ukeketaji, Nyerere Kutwa amesema juhudi zimeongezeka baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa amri ya kutaka vitendo hivyo viwe vimekomeshwa kufikia mwaka 2022.

“Amri ya Rais imetupatia nguvu, na Bodi hii ambayo inasimamiwa na Mwenyekiti aliyeteuliwa na Rais, ndiyo imepewa nguvu kubwa ya kutekeleza amri hiyo ya Rais,” Kutwa amesema.

Afisa anayeshughulikia masuala ya watoto kutoka wilaya ya Kuria West nchini Kenya, Charles Omondi amesema nguvu kubwa imeelekezwa katika kuhamasisha makundi ya rika na jinsia zote kuunga mkono juhudi za kupinga ukeketaji.

Naye Waziri wa Elimu, Utamaduni, Jinsia, Masuala ya Vijana, Michezo na Huduma za Jamii nchini Kenya, Samson Maginga Ng’ariba amesema wameanzisha kamati za kupinga ukeketaji katika kila wilaya, ambazo zinasambaza elimu hadi ngazi ya vitongoji.


Sehemu nyingine ya washiriki mkutanoni

Kwa upande wa Tarime nchini Tanzania, Jeshi la Polisi limetaja vikwazo vya mapambano ya ukeketaji kuwa ni pamoja na watu wengi kutokuwa tayari kujitokeza kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria, dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo.

Wadau hao wamelishukuru Shirika la ATFGM Masanga kwa kuendelea kuwakutanisha wadau kutoka maeneo ya mpakani mwa Tanzania na Kenya, katika juhudi za kukomesha ukeketaji na vitendo vingine vya ukatili wa kijinsia.

“Huu ni mwendelezo wa mikutano ya wadau tunayoiandaa kwa ajili ya kujadili, kuweka mikakati na kufuatilia utekelezaji wake, tangu mwaka 2017,” Meneja Miradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani amesema.

Mkutano huo umehudhuria pia na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Sista Bibiane Bokamba, miongoni mwa viongozi wengine.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages