
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, akizungumza katika mazishi ya kijana wa Chifu Peter Zakaria mjini Tarime, leo Jumatatu.
Tarime
--------------
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano wakati wote kwa maendeleo na ustawi wa taifa.
“Tudumishe amani bila kujali itikadi za vyama vyetu wala koo,” Waziri Nyansaho amesema mjini Tarime leo Jumatatu, Machi 16, 2026, wakati akihudhuria mazishi ya Frank Peter Zakaria ambaye ni kijana wa mfanyabiashara maarufu Kanda ya Ziwa na Chifu wa Koo ya Watimbaru Wilaya ya Tarime, Peter Zakaria.
Waziri huyo alisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo ya jamii na taifa, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha inalindwa na kudumishwa wakati wote.

Waziri Nyansaho akisaini kitabu cha maombolezo. Aliyesimama pembeni yake ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.
Aidha, Waziri Nyansaho aliwasilisha salamu za pole kwa familia ya Chifu Peter Zakaria kwa kuondokewa na kijana wao Frank (41) ambaye alifariki dunia kwa ajali ya gari, Alhmais iliyopita.
Alisema mchango wa Chifu Peter Zakaria katika maendeleo ya jamii ya Tarime, mkoa wa Mara na Kanda ya Ziwa unatambulika na kuthaminiwa.

Waziri Nyansaho akimfariji Chifu Peter Zakaria na familia yake
“Mzee Peter Zakaria ni mfadhili na muumini mwaminifu wa Chama Cha Mapinduzi, hivyo kifo cha mwanaye kinagusa chama chetu… Ukiwa kiongozi, ukiwa mfanyabiashara, wakati ukiwa hai fanya kazi kama vile unakufa siku hiyo hiyo, watendeeni watu mema ili siku ukilala basi jina lako lipate kuishi.
“Tayari nimewasilisha salamu zangu za rambirambi na pia nitawasilisha salamu za Mhe. Rais [Dkt. Samia Suluhu Hassan] hapa,” alisema Waziri Nyansaho na kumwomba Mungu aitie nguvu familia ya Chifu Peter Zakaria kipindi hiki kigumu.

Mazishi hayo yalifanyika nyumbani kwa Chifu Peter Zakaria mjini Tarime na kuhudhuriwa na maefu ya waombolezaji kutoka maeneo tofauti ndani na nje ya wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara.
Ibada ya mazishi hayo iliendeshwa na Padre Aloyce Magige wa Kanisa Katoliki.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Fadhili Maganya, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Christopher Mwita Gachuma.
Wengine ni Wakuu wa Wilaya, Meja Edward Gowele (Tarime), Juma Chikoka (Musoma) na Angelina Marco (Serengeti), Wabunge Esther Bulaya (Jimbo la Bunda Mjini) na Esther Matiko (Jimbo la Tarime Mjini), viongozi wa dini na wafanyabiashara mbalimbali, miongoni mwa wengine.
No comments:
Post a Comment