NEWS

Wednesday 18 August 2021

CEO BRELA awataka maafisa biashara kutofunga biashara




AFISA Mtendaji Mkuu (CEO) wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) nchini, Godfrey Nyaisa (pichani juu) amewataka maafisa biashara kutowafungia wafanyabiashara shughuli zao, kwani kufanya hivyo ni kuchangia kuua uchumi wa nchi.

Badala yake, CEO Nyaisa amewataka maafisa hao kutoa huduma bora na kwa weledi, kutumia busara na kuwa kipimo cha kuwezesha watu kuanzisha na kufanya biashara kwa tija.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano ya sheria ya leseni za biashara, kwa maafisa biashara wa mikoa ya Dodoma, Singida na Morogoro, yanayofanyika kwenye ukumbi wa JK Convention Centre jijini Dodoma.



Amefafanua kuwa maafisa biashara hawapaswi kujikita kwenye ukusanyaji wa mapato pekee, bali pia wana jukumu la kuwaelimisha wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kusajili biashara zao na kupata leseni na kuwafuatilia kwa karibu, ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.

“Muepuke sana kufunga biashara, afisa biashara kazi yako kubwa ni kusimamia wafanyabiashara. Ikiwa utafunga biashara utasimamia watu gani? Hii ina maana huwataki wafanyabiashara,” CEO Nyaisa amesisitiza.

Amesisitiza kuwa huduma bora za maafisa biashara zitawezesha wafanyabiashara wengi kurasimisha biashara, ili kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, au taasisi za kifedha.


Washiriki wakifuatilia mada katika mafunzo hayo

CEO Nyaisa amesema matarajio yake ni kwamba mafunzo hayo yatasaidia kubadili fikra na mitizamo ya maafisa biashara na watendaji wengine wa Serikali na kuwa watoa huduma na msaada kwa wafanyabiashara, ili watakaporudi katika vituo vyao vya kazi, wawe chachu ya uwekezaji, ukuaji na uanzishwaji wa biashara.

“Kuweni watoa huduma na msaada kwa wafanyabiashara, ili ifikapo mwisho wa mwaka kila mmoja ajipime na kujihoji ni watu wangapi aliowezesha kuanzisha biashara. Fuateni watu na kuwawezesha kuanzisha biashara, siyo watu wawafuate ninyi kutaka kuanzisha biashara, na msiwe watu mnaokimbiwa na wafanyabiashara,” amewahimiza maafisa biashara hao.

Kwa upande mwingine, Nyaisa amewataka wafanyabiashara kuondokana na dhana kwamba gharama ya usajili wa majina ya biashara na kampuni ni kubwa, kwani BRELA ni taasisi ya kutoa huduma, hivyo gharama zinazotozwa ni ndogo.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages