NEWS

Thursday 26 August 2021

Kampuni ya KUBATA yazinduliwa rasmiKAMPUNI ya Kuza Uchumi Boresha Afya Tanzania (KUBATA), imezunduliwa rasmi na kuweka wazi mipango yake ya kutoa huduma bora na kuwezesha ukuaji wa uchumi kwa kila mwanachama.

Hafla ya uzinduzi huo imefanyika kwenye ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime mkoani Mara, leo Agosti 26, 2021.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, mfanyabiashara Reuben Mtengi ameupongeza uongozi wa KUBATA, kwa ubunifu wa kuanzisha kampuni hiyo.


Mtengi akizungumza wakati wa uzinduzi huo

Aidha, Mtengi ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kuwa na mbinu bora za kisayansi, maamuzi sahihi, lakini pia kushirikiana na Serikali, ili kutekeleza shughuli zake kwa ufanisi zaidi.

Awali, akisoma taarifa yake kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu (DG) wa KUBATA, Chacha Marwa Getamuru amesema dhima kuu ya kampuni hiyo ni kukuza uchumi na kuboresha afya kwa kutumia kilimo, ufugaji, viwanda, Vyama vya Kuweka na Kukopa (Saccos) na rasilimali watu.


DG Getamuru akizungumza wakati wa uzinduzi huo

“Lengo la kwanza la KUBATA ni kuwa kufikia Januari 2022 iwe imesajiliwa kama kampuni ya umma, itakayounganisha wakulima na wafugaji Tanzania na nje ya nchi na kuwawezesha kulima na kufuga kisasa.
 
"Baada ya mavuno, kampuni itanunua mazao yote na baadaye kuandaa bidhaa zitakazouzwa kwa mawakala wa KUBATA kwa mfumo wa biashara mtandao,” DG Getamuru amesema.

Kwa mujibu wa DG huyo, hadi sasa kampeni ya KUBATA imefanikiwa kuunganisha wanachama na kupata wanahisa mbalimbali na imejipanga kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki na kilimo cha miwa wilayani Tarime.

Baadhi ya wanahisa na wageni waalikwa katika uzinduzi huo

Hata hivyo, DG Getamuru amesema KUBATA inahitaji kupata zana za kilimo kama vile trekta, gari la kusafirisha mazao na bidhaa, baadhi ya vifaa vya ofisini ikiwemo kompyuta mpakato (laptop), wafadhili, mtaji wa kuendesha miradi na fedha za kutengeneza mfumo wa mtandao utakaotumika kuunganisha wanachama wa kampuni na kufanya biashara mtandao.

Baadaye katika hafla ya uzinduzi huo wa KUBATA, mgeni rasmi, Mtengi, ameongoza harambee ndogo ya kuchangia uimarishaji wa kampuni hiyo, ambapo ameanza kwa kuchangia shilingi milioni moja.
 
Miongoni mwa wachangiaji wengine ni Mkurugenzi wa Mara Online, Jacob Mugini aliyetoa shilingi 100,000 na kununua hisa 20 zenye thamani ya shilingi 60,000.


Mugini akikabidhi mchango wake kwa mgeni rasmi


Mugini akizungumza wakati wa uzinduzi huo

(Habari na picha zote: Mra Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages