NEWS

Sunday 8 August 2021

Mkurugenzi JATU atua Mwanza, atoa mrejesho wa mauzo ya hisa
MKURUGENZI Mkuu (DG) wa Kampuni ya JATU (JATU PCL), Peter Isare Gasaya (pichani juu) amekutana na wanachama na wawekezaji wa hisa za kampuni hiyo waliopo Kanda ya Ziwa na kuwapa mrejesho wa mauzo ya hisa.

Mkutano huo umefanyika kwenye ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza leo Agosti 8, 2021, ikiwa ni siku moja baada ya DG Gasaya kukutana na wanachama na wawekezaji wa hisa za JATU PLC jijini Dar es Salaam na kuwapa mrejesho huo.


Mkutano huo jijini Mwanza

DG Gasaya ametumia nafasi hiyo pia kuzishukuru taasisi na wadau wote waliohusika katika mchakato wa kuwezesha mauzo ya hisa za kampuni hiyo kwa umma.

Ametaja taasisi na wadau hao kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Nyingine ni Kampuni ya Archco Limited (Mshauri Mteule), Kampuni ya Mafuru & Co. Advocates (Mshauri wa Sheria) na Kampuni ya Diamond Finacial Services (Wakaguzi wa Hesabu).


DG Gasaya (kulia) na Meneja wa JATU PLC Kanda ya Ziwa, Amperius Rweyimamu katika mkutano wa jijini Mwanza.

“Aidha, tunapenda kutoa shukrani na pongezi za dhati kwa wawekezaji wapya na wadau wote, kwa ushirikiano na imani waliyonayo kwa kampuni ya JATU PLC,” ameongeza.


Mkutanoni jijini Mwanza

Kwa mujibu wa DG Gasaya, mauzo ya hisa za JATU PLC kwa umma yamefanyika kwa mafanikio, ambapo imeuza hisa 15,526,372 sawa na asilimia 104 na kuvuka lengo la kuuza hisa 15,000,000.

Mei 31, 2021, CMSA iliidhinisha maombi ya JATU PLC kuuza hisa 15,000,000 kwa umma kwenye soko la awali, zenye thamani ya Sh bilioni 7.5, kwa bei ya Sh 500 kwa kila hisa, ambapo mauzo ya hisa yalifunguliwa Juni 1, 2021 na kufungwa Julai 15, 2021.

(Na Mwandishi Wetu, Mwanza)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages