
Baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa Kampuni ya Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies wakati wa kukabidhi matofali kuchangia ujenzi wa ofisi ya Kitongoji cha Mjini Kati leo.
Tarime
------------
Kampuni ya Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies, imeendelea kushirikiana na jamii katika kuleta maendeleo - kwa kutoa msaada wa matofali yenye thamani ya shilingi milioni 1.5, kuchangia ujenzi wa ofisi ya Kitongoji cha Mjini Kati, katika kijiji cha Kewanja wilayani Tarime.
Kemanyanki imekabidhi matofali hayo kwa viongozi wa kitongoji hicho leo Agosti 13, 2026, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wa kurejesha kwa wananchi sehemu ya faida yake kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya kijamii katika maeneo ambayo shughuli zake zinafanyika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Nicolaus Mgaya maarufu kwa jina la Chichake, mafanikio ya biashara yanaambatana na wajibu wa kushirikiana na jamii katika shughuli za maendeleo.
Ndiyo maana kampuni hiyo imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha sehemu ya mapato yake yanaelekezwa katika kuchangia juhudi za kufanikisha miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Matofali hayo yanatarajiwa kuwa kichocheo cha kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo ili kurahisisha utoaji wa huduma za kiutawala na kuimarisha shughuli za maendeleo katika kitongoji cha Mjini Kati.
Hivyo, ujenzi wa ofisi hiyo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za kijamii na kiutawala, huku ukiimarisha mazingira ya utendaji wa viongozi wa ngazi ya kitongoji.

Viongozi wa kitongoji hicho wameishukuru Kemanyanki kwa kutoa matofali hayo, huku wakitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kujitokeza kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii.
Kemanyanki Contractors, Manpower & General Supplies ni miongoni mwa kampuni za wazawa zinazonufaika na fursa za zabuni za huduma mbalimbali za kibiashara katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
No comments:
Post a Comment