NEWS

Friday 13 August 2021

MUWASA yamfurahisha Waziri Aweso utekelezaji miradi ya maji




WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso (pichani juu kushoto) ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maji unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), chini ya Mkurugenzi Mtendaji, CPA Joyce Msiru (pichani juu kulia).

Ameyasema hayo jana Agosti 13, 2021 wakati alipokwenda kuzindua ukarabati wa miundombinu ya maji unaotekelezwa na mamlaka hiyo katika mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya, Mara.

“Ninawapongeza sana MUWASA kwa kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maji,” Waziri Aweso amesema wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Obwere mjini Shirati.


Waziri Aweso (aliyevaa skafu) akisoma maandishi ya uzinduzi huo

Amebainisha kuwa Serikali imetenga bajeti ya Sh bilioni 19 kwa ajili ya kutatua changamoto za maji mkoani Mara.

Kutokana na kufurahishwa na utendaji kazi wa MUWASA, Waziri Aweso ametumia nafasi hiyo pia kutangaza kumteua Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, CPA Joyce Msiru kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usambazaji Masi Safi na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji nchini.

“Dada yangu na Mkurugenzi [wa MUWASA] umeweza kuniheshimisha, kulikuwa na miradi kichefuchefu ambayo utekelezaji wake ulikuwa ni mgumu, mradi wa kwanza ni Mugumu [mradi wa maji wa Manchira wilayani Serengeti], kila mtu ambaye anautekeleza unamshinda, nimeweka vidume kweli kweli vimeshindwa.

“Lakini huyu mama nilivyomwambia nenda kautekleze ule mradi, kwake ulikuwa siyo mgumu, lakini tumempa miradi mingi, leo tumekuja kumpa huu mradi wa Shirati, tulimpa siku 30, yeye amefanya kwa siku 21, nani kama Joyce ndugu zangu… huyu mama tumempa kazi ngumu, kila kazi tuliyompa ameweza kuikwamua.

“Kwa mamlaka niliyopewa na kuaminiwa na Rais wangu Samia Suluhu Hassan, ndugu yangu Joyce Msiru ninamteua kuwa Mkurugenzi wa mamlaka za maji zote nchini, kwa sababu hii kazi anaiweza,” Waziri Aweso amesema na kushangiliwa na umati mkubwa mkutanoni hapo.


Waziri Aweso akiwa amejitwisha ndoo yenye maji kabla ya kumtwisha mwanamke aliye jirani yake wakati wa uzinduzi huo

Mbali ya mradi wa Manchira, MUWASA chini ya Mkurugenzi Mtendaji CPA Msiru, imeweza kuhuisha mradi wa maji wa mji mdogo wa Shirati - uliokuwa umesimama kutoa huduma ya maji kwa miaka zaidi ya 10.

Naye Mbunge wa Rorya, Jafari Chege amempongeza CPA Msiru kwa kusimamia utekelezaji mzuri wa miradi ya maji jimboni hapo. Pia ameishukuru Serikali kwa kuiidhinishia wilaya hiyo shilingi bilioni 5.3 kwa ajili ya kugharimia miradi ya maji.


SerikWaziri Aweso (kulia) na Mbunge Chege wakicheza muziki wa asili jukwaajini wakati wa uzinduzi huo

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages