NEWS

Friday 6 August 2021

Naibu Waziri Mabula afungua rasmi nyumba 50 za makazi bora Buhare zilizojengwa na NHC
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amefungua rasmi nyumba 50 za makazi bora, zilizojengwa na Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), kwa gharama ya shilingi bilioni 2.6 katika eneo la Buhare wilayani Musoma, Mara.

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi huo leo Agosti 6, 2021, Dkt Mabula ameipongeza NHC na Bodi yake, kwa utekelezaji na usimamizi mahiri uliofanikisha ujenzi wa mradi wa nyumba hizo katika majengo 25.


Naibu Waziri Dkt Mabula akizungumza wakati wa ufunguzi wa nyumba hizo

Dkt Mabula ameelekeza NHC na Bodi yake kuridhia ujenzi wa shule ya msingi na zahanati ndani ya eneo la mradi huo, vitakavyomilikiwa na serikali, ili kusogeza huduma hizo karibu na wakazi wa nyumba hizo.

Pia, Naibu Waziri huyo ameelekeza NHC kuziwekea nyumba hizo grili kwenye milango, madirisha na kuzijengea uzio, kwa usalama wa wakazi husika na mali zao.


Naibu Waziri Dkt Mabula (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa nyumba hizo.

“Nielekeze tena kwa NHC, miradi mipya mtakayoendelea kuifanya, mhakikishe mnaweka miundombinu rafiki kwa wakazi,” Dkt Mabula ameongeza.

Ametumia nafasi hiyo pia kuipongeza serikali kwa kuipatia NHC fedha zilizogharimia ukamilishaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere katika eneo la Kwangwa, iliyoanza kujengwa mwaka 1975, nje kidogo ya mji wa Musoma.


Naibu Waziri Dkt Mabula (katikati mbele) katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa nyumba hizo.

“Tayari hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za mama na mtoto, hongereni sana NHC, maana mfupa uliomshinda fisi, ninyi mmeuweza,” amesema Naibu Waziri Mabula.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu (DG) wa NHC, Dkt Maulidi Banyani amemweleza Naibu Waziri Mabula kwamba nyumba hizo 50, kila moja ina vyumba vitatu, zimejengwa kisasa kwa kutumia mkandarasi wa ndani na zimewekewa huduma za maji na umeme.

“Hadi sasa nyumba 49 zimepangishwa na moja imeuzwa. Kodi ya pango kwa kila nyumba ni shilingi 132,000 kwa mwezi, na nyumba zote 50 zimejengwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 10, kati ya akari 135 tunazomiliki huku Buhare,” Dkt Banyani amemweleza Dkt Mabula.


DG wa NHC, Dkt Banyani akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa nyumba hizo

Kwa mujibu wa DG huyo wa NHC, ujenzi wa nyumba hizo ulianza mwaka 2014 na kwamba wananchi zaidi ya 500 walipata ajira, achilia mbali walioendesha biashara ndogondogo, wakiwemo mama lishe.

Naye Mjumbe wa Bodi ya NHC, Immaculata Senje amesema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuliongezea shirika hilo mapato na kuwezesha makazi bora kwa wananchi.


Naibu Waziri Dkt Mabula (kushoto mbele) na viongozi mbalimbali wakifurahia ufunguzi rasmi wa nyumba hizo

Wakati huo huo, Naibu Waziri Mabula amegawa hati miliki za ardhi kwa wananchi kadhaa, kisha kufanya mazungumzo na wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi na watumishi wa sekta ya ardhi mkoani Mara, kwa nyakati tofauti leo.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya ufunguzi wa nyumba hizo ni pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mara, Happiness Mtatua, Mwenyekiti wa chama tawala - CCM Wilaya ya Musoma, Benedicto Magiri, Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt Halfan Haule na Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma. Kapteni William Gumbo.

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages