NEWS

Thursday 12 August 2021

Ubadhirifu Tarime Vijijini: RC Hapi aiagiza TAKUKURU kukamata wahusika
MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Salum Hapi (pichani juu) ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani humo, kuchunguza na kukamata watu wote waliohusika kwenye ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Agizo hilo linavilenga zaidi vijiji 11 vinavyopokea mabilioni ya fedha kila mwaka kutoka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, kupitia mpango wa CSR kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kijamii, kama vile elimu, afya, maji na barabara.

RC Hapi ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya jamii katika halmashauri hiyo jana Aogosti 11, 2021, ambapo ameshuhudia viashiria vya ‘upigaji’ wa fedha za miradi hiyo.

Miradi aliyokagua na ‘kunusa harufu’ ya matumizi mabaya ya fedha ni pamoja na ujenzi wa Shule ya Msingi Ntimaro, Shule ya Sekondari ya Nyamongo na Kituo cha Afya Nyamongo.

Ameonesha kukerwa zaidi na mabaki ya nondo 900 na mamia ya matofali na saruji zilizoganda stooni, huku miradi husika ikitajwa kutumia mamilioni ya fedha bila kukamilika.

“Mnanunua nondo mnazidisha mara mbili ya mradi unaohitaji, mifuko ya cement (saruji) mpaka inaganda, pesa mnapewa na mgodi, tofali moja mnanunua shilingi 2,500, tofali nyingi zimebaki.

“Vyumba vitatu vya madarasa nondo 900 zinabaki - watu wameshalipwa pesa, cement zinaganda - watu wameshalipwa pesa. Tarime inatafunwa na watu wachache.

“Huwezi kujenga vyumba vitatu vya madarasa zikabaki nondo 900, huu ni wizi, madarasa yanajengwa tangu [mwaka] 2019 hayajaisha, mimi sitafumbia macho uozo kama huu, sitafumbia macho matumizi mabaya ya rasilimali za umma.

“Takukuru fanyeni upekuzi wa kina kwenye miradi hii, kamata watu wote watakaokuwa wamehusika kutafuna miradi hii, awe amestaafu, awe yuko kazini, au yuko wapi kamata,” RC Hapi amesisitiza.

Ameendelea kusisitiza kuwa lazima hatua kali zichukuliwe dhidi ya ‘wapigaji’ wote katika halmashauri hiyo, kwani vitendo hivyo vinahujumu jitihada zinazofanywa na serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo, lakini pia vinachafua chama tawala.

“Nataka niwahakikishie, hakuna jiwe litakalobaki bila kupinduliwa, kila goti litapigwa, mradi wa kwanza ni uozo, mradi wa pili ni uozo, mradi wa tatu ni uozo.

“Serikali inahangaika, inatunga sheria, inawabana mgodi toeni fedha za maendeleo ya jamii, fedha za CSR zinatolewa mnakula, sasa sisi hatutavumilia jambo hilo, hatuwezi kuvumilia, kwa sababu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi lazima itekelezwe.

“Hii ndiyo kazi aliyotutuma Rais, tutafanya kazi kwa niaba ya wana-Tarime. Hawa wanaokula hii miradi wanaichonganisha serikali na wananchi, wananchi wanaichukia serikali, wananchi wanakichukia chama kinachotawala kwa sababu ya upuuzi huu, ujambazi mkubwa umefanyika hapa.

“Kamada wa Takukuru mkoa fanya kazi yako usimwogope mtu, wa kushika - shika hata kama amestaafu, ili kila mmoja awajibike, hii yote ni kichefuchefu. Mnawezaje kujenga darasa kwa miaka mitatu?

“Waligeuza Tarime kama shamba la bibi. Sijawahi kuona kwenye utumishi wangu wa serikali, madarasa matatu - nodo zinabaki 900, sijawahi kuona matofali yananunuliwa mara mbili ya yanayotakiwa kwenye mradi, cement zinaganda kwenye stoo, na wale walioleta cement wameshalipwa.

“Kamanda wa Takukuru weka kambi hapa, na lisimamie wewe mwenyewe kutoka mkoani, nakujua wewe ni mwadilifu, usicheke na mtu, shika weka ndani,” Mkuu wa Mkoa, Hapi amesisitiza.

Pamoja na hatua hizo, RC Hapi amesema atafikisha hoja ya ubadhirifu huo kwa Waziri wa Nchi - TAMISEMI, ili kuongeza nguvu ya kuwashughulikia wabadhirifu wa mali za umma waliokita katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

“Hii halmashauri ilikuwa imeoza, na tutakwenda kumwomba Waziri wa TAMISEMI, tutafumua halmashauri, tutafumua watendaji wote waliokuwa na mianya na mitandao ya kupiga pesa.

“Mkuu wa wilaya Rais katuletea mpya, mkurugenzi mpya, hawawezi kufanya kazi na mchwa, hatuwezi kufanikiwa, huu mgodi ulipaswa kuifanya Tarime hii iwe imekwisha kuendelea sana, lakini Tarime ni maskini, kuna matumizi mabovu ya pesa Tarime.

“Pesa zimekwisha kutolewa na mgodi, mnanunua material mnavyotaka mpaka mengine yanabaki, na siyo kwa bahati mbaya, kwa sababu wale wanaowa- supply material ni ninyi wenyewe watu wenu, ili wawalipe pesa nyingi mnawambia walete material nyingi.

“Lazima tusafishe hawa mchwa, watu wanatumia huu mgodi kama ni kichaka cha kupiga hela. Rais katuletea mkurugenzi [mpya] tunashukuru, lakini wale wa chini - mtandao wa kupiga hela lazima tuufumue wote kwenye hii halmashauri.

“Mkuu wa wilaya kaa na mkurugenzi na vyombo vingine mtuletee taarifa - watumishi gani ambao hata kama wanahisiwa tu wako kwenye mtandao. Nakwenda kwa Waziri wa Nchi [TAMISEMI], tuifumue Tarime, hapa watu ni wezi, ni wezi, ni wezi.

“DC (Mkuu wa Wilaya) na Mkurugenzi (mpya) tusaidie kusafisha Tarime, tunalia watu wanatafuna pesa tu. Watatapika hiyo pesa, nyie mmeugeuza mgodi kama shamba, halmashauri mmegeuza mgodi kama shamba lenu, siku dhahabu ikiisha wananchi wa hapa watalia na kusaga meno.

“Vijiji vyote 11 vilivyopata pesa na miradi yote iliyoletewa pesa, miamala yote iliyofanyika, tutafanya kazi maalumu kwa ajili ya Tarime. Hii siyo kazi ya Rais, tutaifanya wenyewe, Rais keshafanya kazi yake - katuletea mkutugenzi [mpya], katuletea DC [mpya], hii tutaishughulikia, ni kichefuchefu,” RC Hapi amesisitiza.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages