NEWS

Sunday, 15 February 2026

Mbunge wa Rorya alivyowasilisha hoja Bungeni kuuombea mkoa wa Mara skimu za umwagiliaji



Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, akichangia mjadala Bungeni jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu
Dodoma
---------------

Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege, hivi karibuni aliwasilisha Bungeni hoja nzito kuhusu hali ya kilimo mkoani Mara, akieleza kuwa pamoja na kupakana na Ziwa Victoria, mkoa huo hauna skimu madhubuti za umwagiliaji.

Akichangia mjadala wa kilimo Bungeni jijini Dodoma, Chege alisema ni jambo la kushangaza kuona mkoa wa Mara wenye rasilimali kubwa ya maji ukikosa mafanikio makubwa ya kilimo yanayoweza kuwa mfano wa kuigwa.

“Tunazungumza kilimo, mkoa wa Mara pamoja kuzunguka Ziwa Victoria hatuna skimu kubwa ya kuzungumza leo kama kielelezo cha ukuajji wa kilimo katika mkoa wa Mara,” Chege alisema kwa msisitizo.

Mbunge huyo kijana aliweka bayana hali halisi ya jimbo la Rorya, akisema lina mazingira ya kipekee kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo, lakini fursa hiyo inakwazwa na ukosefu wa skimu kubwa za umwagiliaji.

“Kwa mfano, mimi Rorya nimezungukwa na maji kwa asilimia 77, lakini ninavyozungumza hatuna skimu yoyote ya umwagiliaji tunayojivunia. Katika asilimia 100, nina asilimia 23 peke yake ya nchi kavu, lakini hatuna skimu ya umwagiliaji tunayojivunia,” alisema Chege.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba serikali kupitia Wizara ya Kilimo kufanya upembuzi yakinifu wa haraka katika maeneo ya Mara ili kujenga skimu kubwa za umwagiliaji zitakazosaidia kuinua uchumi wa wananchi.

“Tunatamani mkoa ule tuwe na skimu ambazo zinawainua wananchi kwenye uchumi na zinaleta manufaa kwenye sekta ya kilimo kwa ujumla wake,” alisema Mbunge Chege.

Alisisitiza kuwa si busara kuendelea kuhubiri mapinduzi ya kilimo ilhali baadhi ya maeneo yenye fursa kubwa hayapati msaada wa kitaalamu na miundombinu stahiki.

“Kwa hiyo, ningetamani wizara iangalie namna bora ya kusaidia maeneo yale kwenye kilimo badala ya kubaki tunazungumza kilimo lakini maeneo ambayo yana fursa hayanufaiki na kilimo,” alisisitiza Chege.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages