NEWS

Wednesday 25 August 2021

Vifo vya askari wanne, Rais Samia atuma salamu za pole
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (pichani juu) ametoa salamu za pole kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia vifo vya askari polisi watatu na mmoja wa kampuni ya Security Group Africa (SGA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania, askari hao wameuawa kwa risasi zilizofyatuliwa na mtu aliyekuwa na bunduki, kabla ya yeye naye kuuawa kwa risasi katika makutano ya Barabara ya Kenyatta na Kinondoni jijini Dar es Salaam leo.


Mtu anayesemekana kufyatua risasi zilizoua askari hao

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais - Ikulu, Jaffar Haniu jioni hii, imesema Rais Samia amewataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu, kwani Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vinaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kihalifu.

Aidha, katika taarifa hiyo, Rais Samia amewaombea heri majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao, na amemwomba Mungu kuzipumzisha roho za marehemu mahali pema peponi.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages