NEWS

Wednesday 11 August 2021

Vijiji 44 Tarime Vijijini kunufaika na TASAF
MFUKO wa Mendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) umewapa wawezeshaji na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoa wa Mara, mafunzo yatakayowasaidia kuzitambua kaya maskini zitakazonufaika na mfuko huo sehemu ya pili awamu ya tatu.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwenye ukumbi wa JK Nyerere uliopo Nyamwaga jana Agosti 10, 20211, kiongozi wa timu ya TASAF, Magembe Msika akisoma hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo, Ladislaus Mwamanga amesema vijiji 44 vilivyokuwa vimesalia vitanufaika na mpango huo katika halmashauri hiyo yenye vijiji 88.

“Tathmini ya utekelezaji wa kipindi cha kwanza awamu ya tatu ya TASAF inaonesha kuwa program hiyo imechangia katika kufikiwa kwa azma ya serikali ya kupunguza umaskini nchini, mahitaji ya msingi kwa kaya za walengwa yamepungua kwa asilimia 10 na umaskini uliokithiri kwa kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 12,” Msika amesema.

Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Tarime, Peragia Barozi, Makamu Mwenyekiti wa Halshauri, Victori Mapesa, Diwani wa Kata ya Nyanugu, Tiboche Richard na kiongozi wa timu ya TASAF, Magembe Msika wakiwa katika picha ya pamoja na wawezeshaji wa mpango huo awamu ya tatu katika Shule ya Sekondari JK Nyerere, Nyamwaga jana.

Msika amesema kipindi cha kwanza awamu ya tatu, vijiji na mitaa yote haikufikiwa lakini awamu hii wanalenga kufikia halmashauri zote 184 Tanzania Bara na Visiwani bila kuacha kijiji, mtaa wala shehia, huku kaya yoyote maskini yenye sifa za kuingizwa katika mpango huo ikisajiliwa, baada ya kukubaliwa na wanajamii katika mikutano itakayohudhuriwa na wawezeshaji.

“Kaya zote zinazoishi mazingira duni zitatambuliwa na zile zitakazokidhi vigezo zitaandikishwa katika daftari la walengwa wa TASAF na hatimaye kuanza kupokea ruzuku itakayowezesha kaya hizo kujikimu na kuanzisha miradi itakayowatoa kwenye hali duni,” amesema.


Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo

Aidha, Msika amesema, ili kuepuka kaya ambazo hazina sifa kuingizwa katika mpango huo ambao utafikia kaya milioni 1.4 zenye jumla ya watu zaidi ya milioni saba, lazima wawezeshaji wote ambao ni watumishi wa umma wale kiapo cha uaminifu kwanza.

“Mkazo mkubwa katika kipindi cha pili umewekwa katika kuwezesha kaya zitakazoandikishwa kwenye mpango huo kufanya kazi, ili kuongeza kipato, kuendeleza rasilimali watoto, hususan katika upatikanaji wa elimu na afya, wenye ulemavu na ruzuku ya moja kwa moja itatolewa, au kwa masharti ya kufanya kazi,” Msika ameongeza.

(Imeandikwa na Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages