NEWS

Monday 9 August 2021

Wananchi Tarime wasimulia machungu ya kubomoa nyumba kupisha upanuzi wa barabara




WAMILIKI wa nyumba kando kando ya barabara ya Tarime Mjini – Nyamwaga, wameelezea machungu wanayopitia baada ya kuamua kuzibomoa bila fidia, ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Akizungumza na Mara Online News mjini hapa juzi, kwa niaba ya wamiliki hao, Samwel Werema amesema ingawa wameamua kuvunja wenyewe, wana maumivu makubwa kwani muda waliopewa kubomoa nyumba hizo ni mfupi.


Ubomoaji umeshaanza

Werema ameiomba serikali ifikirie kuwalipa chochote, kwani wengine wana mikopo kwenye taasisi za kifedha na walishatumia kodi za wapangaji.

“Tumeletewa notisi ya kubomoa nyumba ndani ya siku 30, tumeamua kuvunja wenyewe ili maendeleo yafanyike, lakini tunaomba serikali itufikirie kwani tumejenga siku nyingi na tuna hati zilizotolewa na serikali, hivyo tunaomba tufidiwe kwa sababu tumeshtuliwa na watu walikuwa wamechukua mikopo,” amelalamika.
Ubomoaji nyumba ukiendelea

Mara Online News imeshuhudia baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo wakiendelea kuzibomoa kwa unyonge, huku waliokuwa wapangaji wao wakihamisha vitu kwa manung’uniko na wafanyabiashara wengine wakipeleka bidhaa zao majumbani.

Hali hiyo inaonesha wazi kuwa ujenzi wa barabara hiyo sasa ni dhahiri utafanyika bila kikwazo, baada ya wamiliki wa nyumba hizo kuzivunja wenyewe, ingawa awali walitishia kukimbilia mahakamani kuweka zuio la kuzivunja.

(Imeandikwa na Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages