NEWS

Tuesday 31 August 2021

WAMACU kuwekeza viwanda vya kuchakata kahawa kwenye AMCOS




CHAMA cha Ushirika cha Wakulima wa Mara Cooperative Union (WAMACU), kinakusudia kupeleka uwekezaji wa viwanda vidogo vya kuchakata kahawa katika Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).

“Tutafanya uwekezaji huo kufikia Januari 2022, kwa gharama ya takriban shilingi bilioni 1.2 zitakazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),” Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU, Samwel Gisiboye ameiambia Mara Online News ofisini kwake mjini Tarime, juzi.


GM Gisiboye akizungumza na Mara Online News ofisini kwake.

GM Gisiboye ametaja AMCOS zitakazopelekewa viwanda hivyo kuwa ni Kema, Gorong’a, Kangarian, Itiryo, Muriba, Mbogi, Nyakonga na Nyandurumo/ Nkongore za wilayani Tarime.

Meneja huyo amesema WAMACU pia ina mpango wa kujenga kiwanda cha kuchakata kahawa kavu na ya kuoshwa mjini Tarime, kwa gharama ya Sh zaidi ya milioni 400.

“Lakini pia tuna mikakati ya kupeleka miche ya kahawa kwa wakulima mashambani na kuzalisha vitalu vitano vya miche ya kahawa,” ameongeza.


Kahawa shambani

Wakati huo huo, WAMACU imetumia Sh milioni 99 kuzalisha vitalu vya miche 120,000 ya kahawa na Sh milioni 21 kulipia miche 42,000 ya zao hilo kwenda kwa wakulima.

“Tumezalisha vitalu vya miche hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI),” GM Gisiboye amesema.

Kwa mujibu wa GM Gisiboye, hivi karibuni WAMACU imeidhinishiwa mkopo wa Sh milioni 980 kutoka TADB, na tayari imeshapokea Sh milioni 550 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, zikiwemo za kukusanya kahawa kupitia AMCOS.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages