NEWS

Wednesday 18 August 2021

WAMACU yalipa malipo ya pili milioni 113/- kwa wakulima wa kahawa
WAKULIMA wa Mara Cooperative Union (WAMACU) imelipa Sh milioni 113 kwa wakulima wa kahawa, ambazo ni malipo ya pili kwa wakulima waliokiuzia chama hicho cha ushirika zao hilo la biashara msimu uliopita.

“Tulikusanya kahawa kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kila kilo moja, lakini baada ya kuuza na kupata faida, tumewalipa wakulima malipo ya pili ya shilingi 400 kwa kila kilo moja.

“Tumetoa malipo hayo ya pili kwa sababu lengo la ushirika huu ni kuinua wakulima,” Meneja Mkuu wa WAMACU, Samwel Gisiboye ameiambia Mara Online News ofisini kwake jana gosti 17, 2021.


Meneja Gisiboye akizungumza na Mara Online News ofisini kwake.

Kwa mujibu wa Meneja Gisiboye, msimu uliopita WAMACU ilinunua kilo 282,517 sawa na tani 282 za kahawa, kwa gharama ya Sh milioni 339.

Chama hicho cha ushirika kinanunua kahawa za wakulima, kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).

Mkulima wa kahawa, John Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa AMCOS ya Itiryo wilayani Tarime, amesema malipo ya pili yaliyotolewa na WAMACU yamechochea ari ya kilimo hicho kwa wakulima.

“Tangu WAMACU walipe malipo ya pili, katika pitapita yangu nimeona mashamba yanapaliliwa na kuwekewa mbolea kwa nguvu, wakulima wamechangamkia kilimo cha kahawa,” Mwera ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu kutoka kata ya Itiryo.


Kahawa shambani

Wakati huo huo, WAMACU imetumia Sh milioni 99 kuzalisha vitalu vya miche 120,000 ya kahawa na Sh milioni 21 kulipia miche 42,000 ya zao hilo kwenda kwa wakulima.

“Tumezalisha vitalu vya miche hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI),” Gisiboye amesema.

Kwa mujibu wa meneja huyo, hivi karibuni WAMACU imeidhinishiwa mkopo wa Sh milioni 980 katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), na tayari imeshapokea Sh milioni 550 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, zikiwemo za ukusanyaji kahawa kupitia AMCOS.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages