NEWS

Monday 16 August 2021

Wawili wauawa wakitoroka Polisi Tarime-Rorya, 129 mbaroni
JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya limetangaza vifo vya watuhumiwa wawili wa ujambazi na kuwatia mbaroni wengine 129, kati ya Agosti 1 na 15, 2021.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, ACP William Mkonda, waliouawa ni Kihongo Magabe Roboroga (33) na Ngocho Matiko Ndela (34), wote wakazi wa mtaa wa Sabasaba mjini Tarime.

“Walifariki dunia wakiwa wanapelekwa hospitalini baada ya kujeruhiwa kwa risasi miguuni wakati walipojaribu kutoroka chini ya ulinzi wa askari polisi,” ACP Mkonda amewambia waandishi wa habari ofisini kwake, jana Agosti 15, 2021.

Amesema tukio hilo lilitokea Agosti 13, 2021 saa 4:30 asubuhi katika kijiji cha Mtana, nje kidogo ya mji wa Tarime, baada ya watuhumiwa hao kuonesha bunduki aina ya shotgun ikiwa na risasi mbili, inayosadikiwa kutumika katika matukio ya uhalifu.

“Watuhumiwa hao walikuwa ni miongoni mwa wahalifu sugu ambao wamekuwa wakivamia, kuua na kujeruhi walinzi wa maduka katika mji wa Tarime na kupora mali, ambapo walinzi watatu waliuawa na wengine 10 kujeruhiwa kwa kukatwa na vitu vyenye ncha kali,” Kamanda Mkonda amefafanua.


ACP William Mkonda

Ameongeza kuwa watuhumiwa hao pia walionesha vitu walivyopora na kuiba na kuuza baadhi kwa watu tofauti katika maeneo mbalimbali, vikiwemo mabati 156 na vipande vyake 139, mchele kilo 125 na sabuni za unga pakti 135, kila moja yenye uzito wa gramu 500.

Ametaja vingine kuwa ni redio moja aina ya subwoofer na spika zake, solar panel moa, nguo mbalimbali na mikoba ya kike, pikipiki mbili, jiko la gesi, simtank lenye ujazo wa lita 5,000 na gypsum board tano.

“Vitu hivyo vilitambuliwa na wenyewe na pia watuhumiwa saba waliokamatwa na mali hizo wanaendelea kuhojiwa. Aidha, katika kipindi hicho operesheni zilifanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Kipolisi Tarime-Rorya na kupata mafanikio yafuatayo:

“Mashamba 15 ya bangi yenye ukubwa wa ekari 13 na bangi kavu yenye uzito wa kilo 70 ilikamatwa na kuteketezwa kwa moto.

“Pia lita 1,500 za pombe haramu ya moshi (gongo), mtambo, mapipa manne na sufuria mbili vya kutengeneza pombe hiyo, pikipiki saba za matukio ya uhalifu na nyingine 739 zenye makosa ya usalama barabarani zilikamatwa, ambapo 621 zililipiwa faini.

“Lakini pia, ng’ombe 10 na mbuzi watano waliokuwa wameibwa waliokolewa, televisheni moja aina ya Sundar, solar panel tatu na vifaa vya kufanyia uhalifu - panga mbili, nondo mbili na rungu moja vilikamatwa na askari polisi.”ACP Mkonda ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kuendelea kulipatia Jeshoi la Polisi ushirikiano, kwa kuwafichua wahalifu wa makosa mbalimbali, ili wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Pia tunatoa onyo kwa wahalifu wote katika Mkoa wa Kipolisi Trime-Rorya kuacha vitendo hivyo, kwani jeshi letu halitakuwa na muhali (huruma) kwa mhalifu yeyote,” Kamanda Mkonda amesisitiza.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages