NEWS

Tuesday 17 August 2021

Waziri Gwajima akemea ukatili kwa watoto wa kike Tarime



WAZIRI Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima (pichani juu), jana Agosti 16, 2021 amefanya ziara ya kikazi wilayani Tarime, Mara na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike.

Akiwa katika kituo cha kambi okozi cha Shirika la ATFGM Masanga, Dkt Gwajima amewataka wazazi na walezi kuacha kukeketa na kuozesha watoto wa kike kwa nguvu, kwani ni kinyume cha Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

“Hivi unaanzaje kumkeketa mtoto wako kwa nguvu, muelimishe, kinyume na hapo ni ukatilii. Ni sawa na sisi Serikali tuamue kufanya ukatili na chanjo yetu ya UVIKO, tuwakamate ninyi wote tuwachanje,” Waziri Gwajima amesema.


Kutoka kushoto ni Waziri Gwajima akisaini kitabu cha wakeni, Mkurugenzi wa ATFGM Masanga, Sista Bibiane Bokamba Nzali na Meneja Miradi wa Shirika hilo, Valerian Mgani.

Hata hivyo, Waziri Gwajima ameshauri suala la elimu lipewa kipaumbele katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto wa kike.

“Elimu ya mtoto wako ni muhimu. Wekeza kwenye elimu, sheria iwe ya mwisho. Sheria ipo, wale ambao hawataki elimu, sheria hiyo inawahusu. Suala hili ni la Serikali pamoja na jamii,” amesisitiza Dkt Gwajima.

Amepongeza masista wa Upendo wa Mt. Vincent wa Paul kwa kuanzisha Shirika la ATFGM Masanga, linaloendesha kambi okozi kwa watoto wanaokuwa katika mazingira hatarishi ya kukeketwa, chini ya Kanisa Katoliki Dayosisi ya Musoma.

Katika hatua nyingine, Waziri Gwajima ameahidi kusaidia kutatua changamoto zinazolikabili shirika hilo, zikiwemo ukosefu wa bweni kwa ajili ya watoto wanaokimbia ukatili wa kijinsia, gari la kutumika wakati wa kuokoa watoto na kupandisha kituo cha afya cha Bikira Maria Mama wa Tumaini cha Masanga kuwa hospitali.


Baadhi ya Wasichana waliokimbilia kambi okozi ya ATFGM Masangakukwepa ukeketaji, wakimwonesha Waziri Gwajima (hayupo pichani) mabango yanayoonesha mahitaji ya kituo hicho na changamoto zinazowakabili watoto wa kike.

Wanafunzi wa kituo cha ATFGM Masanga na viongozi mbalimbali wakimsikiliza Waziri Gwajima (hayupo pichani) ukumbini.

Awali, Meneja Miradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani amemweleza Waziri Gwajima kuwa vitendo vya ukeketaji na ndoa za utotoni vimekuwa vikikatisha ndoto za elimu kwa baadhi ya watoto wa kike.

“Tunaomba Serikali itusadie kuwapa adhabu kali kwa mujibu wa sheria, wale wote watakaokuwa wamebainika kukatisha masomo watoto na kuwapeleka kwenye tohora,” Mgani amesema katika taarifa yake kwa Waziri Gwajima.

Hata hivyo, Mgani amesema shirika la ATFGM Masanga kupitia kambi yake okozi, limefanikiwa kuokoa watoto zaidi ya 3,800 waliokuwa katika mazingira hatarishi ya kukeketwa, kati ya mwaka 2008 na 2020.


Valerian Mgani (kulia) akisoma risala kwa mgeni rasmi, Waziri Gwajima (kushoto). Katikati ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt Juma Mfanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele amewahakikishia wasichana waliopo katika kambi okozi kutokuwa na wasiwasi kutokana na msimu wa ukeketaji unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.

“Sisi kama wilaya tumejipanga na usalama kwa hao watoto upo “guaranteed’ Kanali Mntenjele amemueleza Waziri Gwajima.

Kauli ya DC huyo imekuja baada ya mmoja wa wasichana waliopo katika kituo hicho kuiomba Serikali mbele ya Waziri Gwajima, kuwalinda dhidi ya vitendo vya kulazimishwa kukeketwa.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages