NEWS

Friday 20 August 2021

Wings Youth Group Nyamongo yawafunda wanafunzi Siku ya Vijana Duniani




KIKUNDI cha Vijana cha Kijamii (Wings Youth Group - WYG) Nyamongo wilayani Tarime, Mara kimeadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwa kuendesha warsha ya kuwajengea vijana 340 mbinu za kufikia mafanikio.

Vijana hao kutoka shule za sekondari za Ingwe, Nyamongo, Kemambo na Maryo, wamekutanishwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Ingwe, nje kidogo ya mji mdogo wa Nyamongo, wiki iliyopita.

Katika warsha hiyo, walimu, wataalamu mbalimbali na wachangiaji wamejikita katika kujadili mada za kuwajengea wanafunzi hao uwezo wa kujitambua, kuthubutu, nidhamu na kufikia mafanikio.



“Mjadala huu ulikuwa shirikishi, wanafunzi waliweza kuuliza maswali na kujibiwa,” Mwenyekiti wa WYG, Yusuph Gesase (pichani juu) ameiambia Mara Online News, muda mfupi baada ya warsha hiyo iliyopewa jina la Career Fair.

Sambamba na hayo, wameendesha harambee ndogo ya kuchanga fedha za kumsaidia mwanafunzi wa kidato cha sita, aliyepata tatizo la kuvunjika miguu, lakini bado akaweza kufanya Mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne.

Wazungumzaji mbalimbali wameahidi kuwazawadia wanafunzi watakaofanya vizuri katika mitihani ya Taifa, kwa masomo ya Sayansi na Hesabu.

Wamehitimisha warsha hiyo kwa kuazimia kwa pamoja kuanza kuthubutu kama vijana, kuwa na nidhamu, malengo na kufikia mafanikio.

Kijana Nicodemus Keraryo ambaye ni mkazi wa Nyamongo na mhitimu wa chuo kikuu, amekipongeza kikundi hicho cha WYG kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani kwa kuwajengea wanafunzi hao uwezo huo.


Nicodemus akizungumza katika warsha hiyo

“Nimefurahi kuona mnawaunganisha vijana wa vijiji vinavyozunguka mgodhi wa dhahabu wa North Mara. Warsha hii ikawe chachu ya mabadiliko yenu katika hatua za kuzitambua na kuzitumia. Nawapongeza vijana wote walioshiriki,” Nicodemus amesema.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages