NEWS

Thursday 23 September 2021

BWIRE INTERNATIONAL SCHOOL: Kisima cha elimu bora Tarime, Mara, Kanda ya Ziwa
“WAZAZI na walezi leteni watoto wenu wapate elimu bora katika mazingira ya kuvutia na wezeshi ya kujifunza kwa weledi hapa Bwire International School.”

Hiyo ni kauli ya Mwalimu Mkuu wa Bwire International School, Reuben Matinde katika mazungumzo maalum na Mara Online News ofisini kwake hivi karibuni, ambaye anajivunia taaluma na matokeo bora ya wanafunzi wake katika mitihani ya kitaifa.

“Hakuna mzazi aliyejutia kumleta mtoto wake kusoma katika shule hii. Tuna kila sababu ya kuwathibitishia Watanzania kuwa shule yetu ni mkombozi wa elimu bora,” anasema.

Bwire International School, ni shule ya kisasa ya bweni na kutwa kwa wanafunzi wa darasa la awali na msingi (darasa la kwanza hadi la 7), yenye mchepuo wa Kiingereza na hadhi ya kimataifa.

Ni mradi mkubwa wa kijamii uliofanikishwa na mwekezaji mzawa, James Marwa Bwire katika eneo la Nyamwaga wilayani Tarime, Mara.Mwalimu Matinde anaitaja Bwire International School kama fursa adhimu ambayo mzazi, au mlezi hapaswi kuikosa kwa ajili ya elimu bora kwa mtoto/ watoto wake.

Mbali na mazingira mazuri, anasema ada zao ni nafuu na rafiki, zinazolipwa kwa awamu tatu wana somo la kompyuta, huduma za uhakika za umeme madarasani, maji, magari ya usafiri, matunda na mboga za majani kwa wanafunzi na walimu.

Anasema wamejiimarisha kuanzia kwenye miundombinu hadi kwa walimu, akitolea mfano matokeo mazuri ya wahitimu wa kwanza wa darasa la saba wa shule hiyo katika Mtihani wa Taifa mwaka juzi.

“Mwaka 2019 shule yetu ya Bwire International School ilifanya mtihani wa Taifa wa kwanza wa darasa la saba na matokeo mazuri yaliiwezesha kushika nafasi ya kwanza kiwilaya, ya 3 kimkoa na ya 51 kitaifa.

“Tunajivunia matokeo hayo, kwani shule zilizoshiriki mtihani huo katika wilaya ya Tarime ni 85, mkoa wa Mara zilikuwa 656 na kitaifa zilikuwa 9,929,” Mwalimu Matinde anafafanua.

Kwa mujibu wa mwalimu huyo, mwaka jana pia shule hiyo ilifanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, kwa kushika nafasi ya pili kiwilaya kati ya shule 109, ya 5 kimkoa kati ya 663 na ya 67 kitaifa kati ya 10,659.

Anafichua siri ya mafanikio hayo kuwa ni utaratibu waliojiwekea wa kuwaweka wanafunzi wote wa darasa la 4, 6 na 7 kwenye mabweni kipindi cha kuelekea mitihani ya Taifa, kwa ajili ya vipindi maalumu vya masomo.

“Lakini pia tumejiwekea utaratibu wa kuanza silabasi mapema. Mfano, silabasi ya darasa la saba tunaanza kuifundisha Oktoba kwa wanafunzi wa darasa la 6 na kuikamilisha Februari wakiwa darasa la 7.

“Baada ya hapo tunaanza kuwapa mitihani mara 3 kwa wiki, yaani kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa hadi kipindi cha mitihani ya Taifa,” Mwalimu Matinde anaongeza.

Anataja siri nyingine ya wanafunzi wa Bwire International School kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kuwa ni kila somo kwa wanafunzi wa darasa la 7 kufundishwa na walimu wawili.“Vilevile walimu wote wanaishi katika mazingira ya shule, hivyo kila wanapohitajika kwenye vipindi vya kufundisha wanafika kwa wakati,” Mwalimu Matinde anaongeza.

Anabainisha kuwa kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 290 wa darasa awali, darasa la kwanza hadi la 6 (ukiondoa 40 waliohitimu la 7), walimu 20, vyumba 14 vya madarasa, maktaba ya kisasa na kwamba wanatarajia idadi ya wanafunzi itaongezeka hadi 400 kufikia Februari mwakani.

“Lugha tunayotumia hapa ni ya Kiingereza tu, Kiswahili wanafunzi wanaongea wakati wa kipindi cha somo la Kiswahili darasani tu, nje ya hapo usipozungumza Kiingereza labda uongee Kichina, au Kifaransa.

“Tunafundisha pia lugha za Kichina na Kifarasa ili kuwajengea wanafunzi wetu uwezo wa kukabiliana na ushindani ya soko la ajira siku za mbeleni,” Mwalimu Matinde anafafanua.

Hata hivyo, licha ya Kiingereza kuwa lugha kuu ya ufundishaji shuleni hapo, Mwalimu Matinde ni mbobezi na mtaalamu mahiri wa kufundisha somo la Kiswahili.

Mwaka 2018 aliweka rekodi ya wanafunzi wake kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwa ufaulu mzuri katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la 7, alipokuwa akifundisha Alliance International School ya mkoani Mwanza.

Mwalimu Matinde anazidi kujivunia mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia ya Bwire International School, ikiwemo lishe bora kwa wanafunzi na mabweni ya kisasa ya wavulana na wasichana.

Anabainisha kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ni kutoka mkoa wa Mara na mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Kwa upande mwingine, Bwire International School imesajili klabu ya michezo mbalimbali kwa ajili ya watoto wa kiume na kike wenye vipaji.“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika tasnia ya michezo hapa nchini Tanzania na nje ya nchi yetu,” Mkurugenzi wa Bwire International School, James Bwire anasema.

Bwire anaona fahari kuwekeza kwenye elimu bora kwa watoto kwa gharama nafuu katika wilaya yake ya kuzaliwa [Tarime], kufadhili baadhi ya wanafunzi na kutengeneza fursa ya ajira kwa wananchi.

Ni ukweli usiopingika kwamba kumekuwa na wazaliwa wa Tarime wenye maendeleo makubwa ya kiuchumi nje ya wilaya na Tanzania, lakini wengi wao wameshindwa kurudi kuwekeza kwenye miradi ya kusaidia jamii, kama anavyofanya Bwire.

Ukiacha shule hiyo ya wilayani Tarime, Bwire anamiliki shule za msingi na sekondari za kisasa jijini Mwanza, zenye historia ya kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages