NEWS

Monday 6 September 2021

Chama cha ushirika cha WAMACU Ltd kusambaza maelfu ya miche ya kahawa kwa wakulimaCHAMA cha Ushirika cha Wakulima wa Mara Union (WAMACU) Ltd kimejipanga kuendeleza uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwa wakulima, kupitia Vyama vya Msingi na Ushirika (AMCOS).

Akiwasilisha taarifa katika kikao kazi maalum cha Bodi ya WAMACU Ltd mjini Tarime Ijumaa iliyopita, Meneja Mkuu (GM) wa chama hicho, Samwel Gisiboye amesema wanaendelea kukamilisha usambazaji wa miche iliyo vitaluni.

“Pia tunaendelea kumalizia maandalizi ya miche ambayo TaCRI (Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania) ilipewa shilingi milioni 99, kwa ajili ya kuzalisha vitalu vine vya miche ambavyo havijakamilika.

“Aidha, fedha iliyopelekwa TaCRI kwa ajili ya ujenzi wa vitalu vinne maandalizi yake yanaendelea vizuri, mbegu ziko vitaluni na miche iliyo tayari kwa ajili ya kwenda shambani ni 30,294,” GM Gisiboye ameongeza.


GM Gisiboye (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa kikaoni. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, David Hechei.

Amesema pia kuna miche 106,377 inayotakiwa kwenda shambani, ambayo WAMACU Ltd imewasilisha ombi la fedha katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kwa ajili ya kulipia gharama ya kuipeleka shambani.

Kwa upande mwingine, GM huyo amesema katika msimu wa 2021/2022, WAMACU Ltd imeanza kukoboa kahawa kupitia kiwanda cha AMIR HAMZA (T) LTD kilichopo Tarime, kwa kupokea malipo ya Sh milioni 9, na tayari kazi hiyo imeshaanza.


Mjumbe akichangia mada kikaoni

“Mpaka sasa, tumeshachakata kahawa safi yenye uzito wa kilo 54,716. Mategemeo yetu kufikia wiki kesho [wiki hii}, tutakuwa tumemaliza tani zote 112,984,” amesema na kuongeza:

“Aidha, chama kinaendelea na ukusanyaji wa kahawa kidogokidogo wakati tukisubiri makusanyo ya mwezi huu Septemba], ambapo tunategemea kupokea kahawa nyingi kuelekea mwishoni mwa msimu wa 2021/2022.”

Katika hatua nyingine, GM Gisiboye amesema WAMACU Ltd imewasilisha katika TADB maombi ya mkopo wa mashine za kuchakata kahawa.


Mjumbe mwingine akichangia mada kikaoni

“Pamoja na gharama za mashine, pia tumewasilisha makadirio ya gharama za ujenzi wa miundombinu na usimikaji wa mashine zote kwa kila AMCOS.

“Hii ni kwa kadiri benki itakavyoona inafaa baada ya kuwa tumepokea ramani na BOQ kutoka kwa Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ikionyesha makadirio yake,” amesema.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages