
Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji Kigera.
Musoma
----------------
Kiwanda cha Nguo Musoma (MUTEX) kilichosimama kwa miaka zaidi ya 10 sasa huenda kikarejea kufanya kazi baada ya kupata mwekezaji wa kukifufua.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji Kigera, alidokeza wiki iliyopita kwamba mwekezaji huyo anatarajiwa kutumia shilingi zaidi ya bilioni 120 kukihuisha.
Hata hivyo, Mbunge Mgore ambaye alikuwa akiwasilisha taarifa ya siku 100 za utendaji wake tangu achaguliwe, alisema bado serikali haijamtaja mwekezaji huyo.
Aliweka bayana kuwa serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha makubaliano na mwekezaji huyo ili iweze kumkabidhi kiwanda hicho ifikapo Juni 2026.
Alisema ameiomba serikali impe mwekezaji ekari 11.7 kati ya 25 za eneo la kiwanda hicho, na ekari 13.3 zinazobaki zitumike kujenga viwanda vidogovidogo vya wananchi.
“Lengo langu ni kuona Musoma inakuwa imara kiuchumi na wananchi wanapata fursa za kuwaongezea kipato,” alisema Mbunge Mgore.
Kufufuliwa kwa MUTEX kunatarajiwa kurejesha uzalishaji wa nguo, ajira kwa wananchi hususan vijana, kuinua uchumi wa Musoma na kuongeza mapato ya serikali.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment