NEWS

Thursday, 16 September 2021

Diwani Mnyanya apiga jeki miradi ya maendeleo Serengeti




DIWANI wa Viti Maalum Tarafa ya Rogoro wilayani Serengeti, Jackline Mnyanya (CCM) ametoa misaada mbalimbali kuunga juhudi za makundi rika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Misaada hiyo ni pamoja na saruji mifuko 10 yenye thamani ya Sh 210,000 aliyokabidhi juzi, kuunga mkono juhudi za makundi rika ya vijana wanaojenga vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Manyata.


Diwani Mnyanya akikabidhi saruji hiyo


Jengo la vyumba vya madarasa shuleni hapo

Kwa upande mwingine, Diwani Mnyanya ambaye pia ni Mlezi wa Kata za Machochwe, Sedeco, Mbalibali na Mugumu, amekabidhi msaada wa mavazi ya kurinia asali, yenye thamani ya Sh 300,000 kwa kikundi cha Uvima kilichopo kijiji cha Machochwe.



Diwani Jacline Mnyanya (katikati) mara baada ya kukabidhi vifaa vya kurinia asali.


Katibu Hamasa wa UVCCM Wilaya ya Serengeti, Chief Mosabi Francis (katikati) akiwa na baadhi ya wanakikundi cha Uvima kilichopewa msaada wa vifaa vya kurinia asali.

Pia amekabidhi msaada wa mipira miwili kwa ajili ya vijana, ambayo ni ahadi iliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti, Esther Mong'ori wakati wa ziara yake katani hapo.


Akizungumza na wananchi wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Diwani Mnyanya ameahidi kuendelea kushirikiana nao na Diwani wa Kata ya Machochwe, Joseph Muhengete katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwepo kupata milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Machochwe.


Diwani Muhengete akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya misaada hiyo.

Wananchi wa kata hiyo wamewapongeza madiwani hao kwa ushirikiano wa dhati wanaoonyesha katika kuwaletea maendeleo ya kisekta.


Msafara wa madiwani hao umewashirikisha Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Serengeti, James Lugendo na Katibu Hamasa wa Umoja huo wa Wilaya hiyo, Chief Mosabi Francis, miongoni mwa viongozi wengine wa Chama na Serikali.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages