NEWS

Saturday, 17 January 2026

RC Mtambi, Machifu Gachuma, Peter Zakaria wakutana na vijana wa Tarime



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (kulia), Chifu wa Koo ya Wakenye, Christopher Mwita Gachuma (wa pili kushoto), Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zakaria (kushoto), wakifurahia kuimba na kucheza na msanii wa muziki, walipokutana na vijana wa Tarime kwenye Hoteli ya CMG, jana Ijumaa.

Na Christopher Gamaina
Tarime
-----------

Vijana wa wilayani Tarime wameshauriwa kubadilika kifikra na kimatendo, ikiwemo kulinda amani ili fursa zaidi za kimaendeleo zifunguke katika eneo hilo na kutengeneza ajira zitazowakwamua kiuchumi.

Ushauri huo ulitolewa na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, na Machifu wa koo za kabila la Wakurya, walipozungumza na vijana takriban 500 kwenye Hoteli ya CMG mjini Tarime, jana Ijumaa.

Mkutano huo ulioandaliwa na Chifu wa Koo ya Wakenye, Christopher Mwita Gachuma, na kuhudhuriwa pia na Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zakaria, na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl. Saul Mwaisenye.


Sehemu ya vijana hao wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Mkoa

Katika hotuba yake, RC Mtambi alisisitiza kuwa fursa nyingi za kiuchumi na ajira zitafunguka Tarime ikiwa kila kijana atabadilika kwa kuepusha na kukemea mambo yanayoichafua wilaya hiyo inayopakana na nchi ya Kenya.

“Badilikeni kifikra na kivitendo. Fursa zitafunguka kwa ninyi kutoichafua Tarime. Utulivu ukiwepo kwenye jamii kila kitu kitafunguka. Ipende Tarime, Ipende Mara,” aliwambia vijana hao.


RC Mtambi akisisitiza jambo kwa vijana hao

RC Mtambi aliwasisitiza vijana hao kuipenda Tarime na Mara mithili ya mboni za macho yao na kuepuka vitendo visivyofaa, la sivyo watakuwa wanajichimbia kaburi lao wenyewe.

Hata hivyo, aliahidi kushughulikia malalamiko waliyowasilisha kwake, ikiwemo kubaguliwa kwenye fursa za kujipatia kipato, kunyimwa mikopo ya fedha inayotolewa na halmashauri, kunyanyaswa na askari polisi na kukandamizwa na mamlaka za kodi.

Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa mkoa aliuagiza uongozi wa wilaya ya Tarime kuhakikisha kuwa mafundi ujenzi wenyeji wanapewa kipaumbele katika miradi inayotekelezwa ndani ya wilaya hiyo.

“Kazi za ujenzi zifanywe na mafundi ambao ni wakazi wa Tarime, mafundi watachukuliwa kutoka maeneo mengine kama hapa hawapo,” aliagiza RC Mtambi.


Vijana mkutanoni

Pia, RC Mtambi aliahidi kuanzisha utaratibu wa kukutana na vijana wasanii waliopo Tarime katika tamasha maalum kila mwanzo au mwisho wa mwezi ili kuwapa fursa ya kuonesha vipaji vyao na kuangalia namna ya kuwasaidia kuvikuza na kuviendeleza.

“Tuwe tunakutana na vijana waoneshe vipaji, vikiwemo vya ‘kuchana mistari’. Kwenye matamasha hayo kuwepo na nyama choma na kichuri watu wanunue wale,” alisema RC Mtambi na kuwashukuru vijana hao kwa kujitokeza kwa wingi kuwasilisha kero zao.

Aidha, kiongozi huyo wa mkoa aliwashukuru Machifu wa Koo za Wakenye na Watimbaru, Gachuma na Peter Zakaria, kwa namna wanavyojitolea kushirikiana na serikali kusaidia jamii kwa hali na mali.

Kwa upande wake, Chifu Gachuma ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama tawala – CCM, alimpongeza RC Mtambi kwa kukutana na vijana hao akisema ni mwanzo mzuri wa kuelekea kwenye ufumbuzi wa changamoto zao.

“Huu ni mwanzo mzuri - tuuendeleze ili vijana hawa ndoto zao ziweze kutimia. Vijana bado mnahitaji maisha, mna safari ndefu na ili mfike salama na muishi vizuri jengeni mahusiano mazuri na serikali,” alisema Chifu Gachuma.


Chifu Gachuma akizungumza katika mkutano huo

Kuhusu ahadi ya RC Mtambi ya kukutana na vijana wasanii katika tamasha maalum kila mwezi, Chifu Gachuma aliahidi kushirikiana nan a kiongozi huyo wa mkoa katika kufanikisha hilo.

“Niko tayari kushirikiana na Mkuu wa Mkoa kufanikisha hili. Ninawaahidi tutawasapoti wasanii wote wa Tarime, tunataka Tarime inayoheshimika, tunataka vijana wa Tarime wanaojitambua na kuaminika,” alisisitiza Chifu huyo wa koo ya Wakenye.

Naye Chifu wa Koo ya Watimbaru, Peter Zakaria, aliwataka vijana hao kutokubali vishawishi vya kushiriki kwa namna yoyote ile vitendo vya uvunjifu wa amani katika jamii.

“Tuepuke vurugu tuwe watu wema, tuache ukorofi ule wa zamani. Hata mimi nilikuwa mkorofi zaidi yenu lakini nimebadilika - nimekuwa mtu mwema ninasaidia jamii,” Chifu Zakaria aliwambia vijana hao.


Chifu Peter Zakaria akiwapa vijana hao ushauri

Vilevile, Chifu Zakaria ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wilayani Tarime, aliwahimiza vijana hao kutii maelekezo ya serikali sambamba na kujenga mahusiano mema na vyombo vya usalama, hususan Jeshi la Polisi.

Awali, vijana hao walipewa nafasi ya kueleza mbele ya viongozi hao kero na maoni yao kwa serikali, ambapo walitaja ukosefu wa ajira kama tatizo kuu linalowakabili.

Walilalamikia pia ukosefu wa soko la kazi za wasanii, viwanja bora vya michezo na wafadhili wa ligi, kunyanyaswa na askari polisi na kunyimwa mikopo ya fedha inayotolewa na halmashauri.

Kutokana na hali hiyo, waliomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapa misaada ya mitaji na vitendea kazi kwa wale waliojianzishia shughuli za ujasiriamali kama vile kilimo, bodaboda, uuzaji wa chipsi na ufugaji wa kuku na samaki kwenye vizimba.


Sehemu ya vijana hao mkutanoni

Lakini pia, waliomba serikali kuelimisha vijana wa Tarime kuhusu fursa za kiuchumi zilizopo na kuhakikisha ajira zinatolewa bila ubaguzi wala upendeleo wowote ule.

Zaidi ya hayo, vijana hao waliomba serikali kuangalia uwezekano wa kujenga kituo cha utalii katika mji wa Sirari uliopo mpakani na nchi ya Kenya, kwa ajili ya kuonesha na kutangaza tamaduni, sanaa, mila na desturi nzuri za wenyeji wa Tarime.

Mwisho, waliwashukuru RC Mtambi, Machifu Gachuma na Peter Zakaria kwa kutenga muda wao kwa ajili ya kukutana nao, kusikiliza changamoto zao na kuwatia matumaini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages