NEWS

Wednesday 22 September 2021

Mikoa sita yakabidhiwa magari ya kufuatilia afya na usafi wa mazingira, Waziri Gwajima ataja vigezo vilivyotumika




WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Dorothy Gwajima, amekabidhi magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli za afya na usafi wa mazingira kwenye mikoa sita nchini.

Mikoa hiyo ni Kagera, Mara, Manyara, Tabora, Songwe na Mtwara, ambapo magari hayo yamenunuliwa kupitia mfumo wa Lipa kwa Matokeo, ikiwa ni programu za afya na yamekuwa yakitumika kwa shughuli nyingine, huku shughuli husika yakitumika kwa asilimia 25.

Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dodoma, leo Septemba 22, 2021.


Waziri Gwajima

“Tunaanza sensa ya kiwango gani magari yanayopelekwa kusimamia programu za afya yanatumikaje huko yanakokwenda, hatusemi sekta ya afya isiwe na ushirikiano na sekta nyingine, tunataka uwiano katika matumizi ya magari hayo na kazi gani linafanya kusaidia sekta nyingine, maana zote ni sekta za Serikali,” Waziri Gwajima amesema.

Amefafanua kuwa Wizara inatekeleza programu ya huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira, yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira vijijini, inayotekelezwa kwenye halmashauri 86 katika mikoa 17 nchini.


Waziri Gwajima (katikati) akikabidhi funguo kwa mmoja wa madereva wa magari hayo.

Dkt Gwajima amebainisha kuwa mikoa hiyo imechaguliwa kwa kuzingatia vigezo vya hali duni ya upatikanaji wa huduna za maji na usafi wa mazingira, kiwango cha umaskini na kiwango cha juu cha udumavu wa watoto.

Amesema kwamba kupitia programu hiyo, mikoa na halmashauri zimeendelea kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii, na kwamba kwa mwaka wa fedha 2020/21, imetekelezwa katika vituo 873 vya kutolea huduma za afya nchini.



Aidha, Dkt.Gwajima amesema Serikali imenunua pikipiki 138 ambazo tayari zinatumiwa na maafisa afya ngazi ya kata, kama sehemu ya utatuzi wa tatizo la usafiri na kwamba yatanunuliwa magari mengine matano.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara hiyo, Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima, amesema magari hayo yamegharimu shilingi zaidi ya milioni 646.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages