NEWS

Monday, 15 June 2026

Mara: Yametimia Uwanja wa Ndege Musoma, ndege za abiria kuanza kutua Julai 2026



Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (aliyevaa shati jeupe), akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, wakati wa uzinduzi wa majaribio ya kuruka na kutua kwa ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma, wiki iliyopita.

Na Mwandishi Wetu
Musoma
----------------

Hatimaye yametimia. Ndivyo tunavyoweza kuelezea uzinduzi wa majaribio ya kuruka na kutua kwa ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma, mkoani Mara baada ya huduma za usafiri wa anga katika uwanja huo kusimama kwa miaka minane.

Uzinduzi huo ulifanyika wiki iliyopita, mgeni rasmi akiwa Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ambaye aliahidi kuwa ndege za abiria zitaanza kutua katika uwanja huo Julai, 2026.

Waziri Mbarawa alitumia nafasi hiyo pia kuliagiza Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuharakisha utaratibu wa kuuingiza Uwanja wa Ndege Musoma kwenye ratiba za ndege za abiria ili wananchi wa mkoa wa Mara waweze kutumia usafiri huo.

“Ninaiagiza ATCL kuhakikisha kuwa inauingiza Uwanja wa Ndege Musoma katika ratiba za ndege haraka iwezekanavyo, ili huduma za usafiri ziweze kutolewa kwa wananchi,” alisema.

Alisema majaribio ya utayari wa viwanja vya ndege Musoma na Shinyanga yanaashiria kukamilika kwa sehemu muhimu za miradi ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu hiyo tayari kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Vilevile, Waziri Mbarawa alizielekeza taasisi zinazohusika na mradi wa ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Musoma ambazo ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege (TAA) na wakandarasi kukamilisha sehemu iliyobaki katika mradi huo kwa mujibu wa mkataba wa utekelezaji.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alisema kuzinduliwa kwa majaribio ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma ni maendeleo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mara ya mwisho ndege kubwa kutua katika uwanja huu ilikuwa ni Machi 2018, ambapo ndege ya Precision Air yenye uwezo wa kubeba abiria 45 ilifanya safari yake ya mwisho katika uwanja huu,” alisema RC Mtambi.

RC Mtambi aliwataka wananchi wa mkoa wa Mara kuchangamkia fursa za kutumika kwa uwanja huo kwa kuanzisha na kukuza shughuli zao, ili kuimarisha uchumi wao kwani watakuwa na uwezo wa kusafiri na kusafirisha mizigo yao kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kwa sasa wananchi na wafanyabiashara wana uwezo wa kusafiri kwa muda mfupi kufika maeneo mbalimbali, jambo ambalo likitumika vizuri linaweza kuchechemua fursa nyingi za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAA, Abdul Mambokaleo, alisema mradi wa ukarabati na upanuzi wa uwanja huo ulianza kutekelezwa mwaka 2021 kwa gharama ya shilingi bilioni 35.

Mambokaleo alieleza kuwa mradi huo pamoja na mambo mengine, umeboresha njia ya kuruka ndege kutoka mita 1,600 za changarawe yenye uwezo wa ndege za abiria 45 zilizokuwepo hadi mita 1,750 za lami zenye uwezo wa kuwezesha ndege za abiria 80 kutua na kuruka katika uwanja huo.

Aidha, Mambokaleo aliahidi kuwa TAA baada ya kulipa fidia kwa wanachi, itaanza kujenga kwa kasi jengo la abiria katika uwanja huo na kukamilisha majengo mengine ya kutolea huduma katika mradi huo wakati huduma nyingine zinaendelea kutolewa.

Uboreshaji na upanuzu wa Uwanja wa Ndege Musoma unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika mkoa wa Mara.

Uwanja huo utawezesha ndege kubwa kutua katika mji huo na hivyo kurahisisha safari kwa watalii wanaotembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mkoa huo, ikiwemo hifadhi bora Afrika - Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Hafla ya uzinduzi wa majaribio ya kutua na kuruka kwa ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma pia ilihudhuriwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, viongozi na watendaji wa taasisi za umma, wabunge, viongozi wa CCM mkoa wa Mara, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida.

WaziriMbara wa akisalimiana kwa kushikana mikono na kada wa CCM, Nicolaus Mahando Mgaya - maarufu kwa jina la Chichake ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kemanyanki Contractors Manpower and Supply Company Ltd, wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa majaribio ya kuruka na kutua kwa ndege katika Uwanja wa Ndege Musoma.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages