NEWS

Wednesday 8 September 2021

Maadhimisho Siku ya Mara: Miti 16,000 kupandwa Tarime




MITI 16,000 ambayo ni rafiki kwa vyanzo vya maji na mazingira inatarajiwa kupandwa katika vijiji vya Mrito na Kerende wilayani Tarime, wakati wa maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara mwaka huu.

Pia, vigingi 60 vitawekwa kila kimoja umbali wa mita 60 kutoka ukingo wa Mto Mara, kwenye eneo lenye urefu wa kilomita tano katika vijiji hivyo.

Hayo yameelezwa na maofisa wa Serikali, wakiwemo kutoka Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), katika kikao cha kuhamasisha maadhimisho hayo kwa viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na tarafa kijijini Mrito leo.


Viongozi hao kikaoni

Sherehe za maadhimisho ya 10 ya Siku ya Mara zitafanyika Septemba 15, 2021 wilayani Tarime, yakibeba kaulimbiu inayosema "Tuhifadhi Mto Mara kwa Utalii na Uchumi Endelevu".

“Tuna wajibu wa kutunza na kuhifadhi mto huu [Mara], una faida nyingi,” Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Dakio la Mara, John Ngawambala amesema.


Ngawambala (aliyesimama) akizungumza kikaoni

Aidha, Ngawambala amewasisitiza wananchi kuzingatia katazo la shughuli za binadamu ndani ya mita 60 kutoka ukingo wa mto, ili kuepuka madhara mbalimbali kwa watu na mto huo.

Adam Renatus kutoka LVBWB, amesema uwekaji wa vigingi unalenda kulinda kina na ubora wa maji ya Mto Mara.


Renatus akisisitiza jambo kikaoni

Naye Lazarus Butilikwa kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, amesema wameona umuhimu wa kuhamasisha maadhimisho ya Siku ya Mara kupitia kwa viongozi hao, kwa kuwa ndio wasimamizi wa utekelezaji wa mipango ya Serikali.


Butilikwa (aliyesimama) akizungumza kikaoni

Afisa Tarafa ya Ingwe, James Yunge, amewataka viongozi hao kuwapa ushirikiano wa dhati wataalamu watakaokwenda kupanda miti na kuweka vigingi kwenye mpaka wa hifadhi ya Mto Mara.

Siku ya Mara imekuwa ikiadhimishwa na nchi za Tanzania na Kenya kwa pamoja, chini ya uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) yenye makao yake Kisumu, Kenya.

Hata hivyo, mlipuko wa virusi vya Korona unaripotiwa kuathiri maadhimisho hayo kwa miaka ya hivi karibuni, huku kila nchi ikiadhimisha kivyake.


Mto Mara humwaga maji yake kwenye Ziwa Victoria upande wa Tanzania

Kwa kutambua umuhimu wa ikolojia ya Mara, kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda. Mei 4, 2012 kiliazimia Septemba 15 kila mwaka kuwa Siku ya Mara.

Maadhimisho hayo hufanyika kipindi cha msimu wa nyumbu kuvuka Mto Mara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania na kuingia mbuga ya Maasai-Mara, Kenya.


Nyumbu wakivuka Mto Mara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Mbali na kuchangia uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania na Kenya.

Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mara yalifanyika mwaka 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania yalifanyika mwaka 2013 katika mji wa Mugumu, wilayani Serengeti.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages