NEWS

Monday 20 September 2021

Ngicho ateta na wanahabari Mara, awataka kutangaza fursa za kiuchumi




MFANYABIASHARA ya madini, Marwa Daudi Ngicho (pichani juu aliyesimama) amehutubia mkutano wa waandishi wa habari mkoani Mara na kuwahimiza kutumia taaluma yao kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo ili kuvutia wawekezaji.

Katika hotuba yake kwenye mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Matvilla Beach mjini Musoma leo Septemba 20, 2021, Ngicho amesema wanahabari wana nafasi kubwa ya kuonesha mkoa huo ulivyo sehemiu bora ya kuishi na kuwekeza.


Washiriki mkutanoni

“Mara kuna mambo mengi mazuri ya kuandika, tuandike habari za kuvutia wawekezaji, kama vile fursa za kuwekeza kwenye sekta za viwanda na madini,” amesisitiza.

Ngicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, ametumia fursa hiyo kuvipongeza vyombo vya habari vya blugu ya Mara Online News na gazeti la Sauti ya Mara, kwa kazi nzuri ya kuhamasisha utalii wa ndani katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Boresheni habari zenu zitapendwa, hasa zinapokuwa za kweli. Mara Online News na gazeti la Sauti ya Mara vinafanya vizuri ya kutangaza utalii, mimi ninalipongeza kwa kazi nzuri sana na wananchi wameanza kuhamasika kufanya utalii wa ndani katika Hifadhi ya Serengeti,” amesema.


Ngicho amebainisha kuwa yeye kama mfanyabiashara ya madini, anatambua na kuthamini mchango wa waandishi wa habari katika kusukuma maendeleo ya jamii.

Aidha, amesema uwekezaji wake kwenye sekta ya madini umetengeneza ajira kwa vijana wengi, wakiwemo waliokuwa wawindaji haramu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kuna vijana wengi nimewapa ajira wakaacha uwindaji,” amesema.

Pia Ngicho amewataka wanahabari hao kuandika habari zinazojenga umoja na mshikamano wa wananchi ndani ya mkoa wa Mara, ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Mkoa wetu unahitaji umoja na waandishi wa habari wenye maadili, kwani wasio na maadili wanaweza kutugawa vipande vipande,” amesisitiza.

Katika mkutano huo, Ngicho ameafuatana na Diwani wa Kata ya Nyanungu kutoka Tarime, Tiboche Richard ambaye ametoa wito kwa jamii kuwapa wanahabari ushirikiano ili kuboresha utendaji kazi wao.


Ofisa wa UTPC, Victor Maleko (kushoto) akizungumza mkutanoni

Mkutano huo ulioratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara (MRPC), ulihudhuriwa pia na Ofisa kutoka Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Victor Maleko na Wakili Daudi Mahemba, miongoni mwa wadau wengine.


Wakili Mahemba (kushoto) akiwasilisha mada mkutanoni

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages