NEWS

Thursday 23 September 2021

Sababu za kahawa inayolimwa Tarime kuteka soko la dunia

Kahawa safi ya Arabica inayolimwa Tarime

TARIME inaweza kuwa moja ya wilaya tajiri, yenye wananchi wenye kipato kizuri nchini, kwani imejaaliwa ardhi inayostawisha kahawa aina ya Arabica, inayotamba katika soko la dunia.

Taarifa zinasema soko la kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime ni kubwa kuliko uzalishaji, hali inayoifanya kuwa bidhaa adhimu kwenye soko la dunia, hususan katika mabara ya Ulaya, Amerika na Asia.

Kahawa inayozalishwa Tarime inaelezwa kuwa na ladha halisi (natural taste) kutokana na sababu zinazotajwa na watalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).

Kahawa aina ya Arabica iliyovunwa

“Sababu ya kwanza ni matumizi madogo ya viuatilifu, yaani Tarime ni ndiyo wilaya ya mwisho Tanzania kwa matumizi ya viuatilifu,” Meneja wa TaCRI Kada ya Ziwa, Almas Hamadi anasema katika mahojiano maalum na Mara Online News mjini hapa, hivi karibuni.

Hamadi anasema mlaji hawezi kufurahia uzuri wa kahawa ambayo inalimwa katika eneo leye matumizi makubwa ya viuatilifu.

“Sababu ya pili ya kahawa ya Arabica kuwa bora katika soko la dunia, ni matumizi madogo ya mbolea za viwandani,” anaongeza.


Meneja Hamadi (kulia) akizungumza na mwandishi wa makala hii, Jacob Mugini.

Anafanunua kuwa hakuna matumizi ya mbolea yanayoweza kuharibu ubora wa udongo unaofaa kwa uzalishaji wa kahawa aina ya Arabica katika wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Hamadi, inakadiriwa kuwa katika wakulima 10, ni wawili wanaotumia viuatilifu wilayani Tarime.

Mkulima wa kahawa shambani

Aidha, Hamadi anasema mfumo mzuri wa uzalishaji na uchakataji wa kahawa ya Arabica wilayani Tarime, unachangia ubora unaotakiwa katika soko la dunia.

“Uchakataji wa Arabica ngumu (hard Arabica) unasababisha uwepo wa ladha halisi ya kahawa ikiwa na virutubisho vyake vyote kwenye mbegu,” Hamadi anasema.



Wataalamu wa kilimo cha kahawa kutoka serikalini wanasema wilaya ya Tarime ni potential (fursa muhimu) kwa uzalishaji wa kahawa ambayo ‘haikamatiki’ kwenye soko la dunia.

“Tarime imebarikiwa kuwa na udongo wa volkano, misimu miwili ya mvua na mazingira yaliyopo, vyote hivi vinaifanya kuwa sehemu sahihi ya kilimo cha kahawa aina ya Arabica,” Mkaguzi wa Kahawa Wilaya ya Tarime, Stanley Rubalila anasema.

Hivyo kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime imeendelea kuwa na soko kubwa katika mataifa yaliondelea duniani ikiwemo Marekani na Uingereza, huku uzalishaji wake ukiwa haukidhi mahitaji ya soko.

“Mfano sasa hivi kuna mnunuzi anayehitaji tani 200 za Arabica kutoka Tarime kwenda Marekani, lakini haitoshi, bado anakusanyiwa,” Hamadi anadokeza.

Mkulima wa kahawa shambani

Mahitaji ya kahawa hiyo katika soko la dunia yameleta neema kwa wakulima, kwani yamechochea ushindani kwa wanunuzi, ingawa wengi wao waliripotiwa kutoa bei kandamizi iliyochangia kufifisha uzalishahi wa zao hilo miaka ya nyuma.

Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Mara Cooperative Union (WAMACU) kimepeta leseni ya kuuza zao hilo moja kwa moja katika soko la dunia, hatua inayoelezwa kuwa na faida kwa wakulima, ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Ushirika wa WAMACU unakusanya kahawa kwa wakulima kupitia Vyama Vya Msingi na Ushirika (AMCOS), kisha kuiuza katika soko la nje.


Kahawa shambani

“WAMACU ina leseni ya kuuza kahawa kwenye masoko ya nje, kama vile UK (Uingereza) na Marekani,” Meneja Mkuu wa WAMACU, Samwel Gisiboye ameiambia Sauti ya Mara ofisini kwake, hivi karibuni.

Anaongeza “Mwaka jana tumeuza kahawa kwa kampuni ya Continental Trade Commodity Services (CTCS) ya UK na mwaka huu tumeuza kwa kampuni ya Volcafe ya Marekani kupitia kampuni yake tanzu ya Tylor Winch.”

Gisiboye anasema itachukua takriban misimu miwili kumkusanyia mnunuzi huyo wa Marekani kiasi cha kahawa anayotaka kulingana na mkataka waliofunga na WAMACU.
Gisiboye akizungumza na Mara Online News ofisini kwake

Kwa upande wa Ulaya, kahawa ya Arabica inayolimwa Tarime pia inauzika vizuri katika nchi za Uholanzi, Ugiriki, Uhispania na Ujerumani. Mbali na Marekani, kahawa hiyo ina soko zuri Costa Rica na Colombia.

Mkakati wa kuongeza uzalishaji
Mbali na kununua kahawa kupitia AMCOS, ushirika wa WAMACU umeanza kuwekeza katika uzalishaji wa miche ya kahawa na kuigawa kwa wakulima, baada ya kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

“Hadi sasa tumetumia shilingi milioni 120 kwenye uzalishaji wa miche bora ya kahawa na mwaka huu tumepanga kutumia milioni kadhaa kuzalisha miche na kuisambaza kwa wakulima ili kupanua uzalishaji,” Gisiboye anasema na kubainisha kuwa WAMACU inashirikiana na TaCRI kuzalisha miche hiyo.

Miche bora ya kahawa

TaCRI itakavyoongeza uzalishaji
Lengo ni kuzalisha tani 15,000 za kahawa ili kukidhi mahitaji ya soko kufikia mwaka 2025.

“Mpaka sasa kuna miche zaidi ya milioni 2.5 amabyo imepandwa katika mashamba wilayani Tarime, lengo ni kuongeza miche mipya milioni tatu. Hii inaweza kusadia kukidhi mahitaji ya soko,” Meneja huyo wa TaCRI Kanda ya Ziwa anasema.



Gisiboye anaongeza “Wakulima wapo tayari kuongeza uzalishaji na msimu huu tuna miche laki tatu ya kupanda kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB),” Hamadi anasema, akiitaja TCB na WAMACU kama wadau muhimu ambao kwa sasa wanaunganisha nguvu kuongeza uzalishaji wa kahawa ya Arabica wilayani Tarime.

Meneja Mkuu wa WAMACU, Gisiboye anasema kwa sasa wananunua kahawa kwa bei ya Sh 1,600 kwa kilo moja, ikiwa imepanda kutoka Sh 1,400 msimu uliopita.



“Sisi tunakusanya kwa cash (kulipa fedha taslimu) na lengo la ushirika ni kumnyanyua mkulima, ndio maana kwa mara ya kwanza wakulima wa kahawa Tarime walipokea malipo ya pili ya shilingi 400 kwa kilo moja msimu uliopita,” anasema.

WAMACU imetumia Sh milioni 113 kufanya malipo hayo ya pili, baada kuuza kahawa na kupata faida.

“Tumetoa malipo ya pili kwa sababu lengo la ushirika huu ni kuinua wakulima,” Gisiboye anasisitiza.

Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU, David Hechei anatoa wito kwa wakulima kutumia fursa zilizopo kuongeza uzalishaji wa kahawa ya Arabica.


David Hechei

“Hii ni fursa ya aina yake kwa wakulima. Ujumbe wangu ni kwamba tuendelee kupanua uzalishaji kwa ubora wa hali ya juu,” Hechei anasema.

(Na Jacob Mugini wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages