NEWS

Thursday 23 September 2021

Ufunguzi Barabara ya Mogabiri – Nyarwana kuipaisha Tarime, Waitara aipa kongole TARURA




NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara leo Septemba 22, 2021 amekagua na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ufunguzi wa Barabara ya Mogabiri – Nyarwana, yenye urefu wa kilomita 5.6 wilayani Tarime, Mara.

Mradi huo unatekelezwa na mkandarasi mzawa, M/S EDOS Limited, chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Tarime.

Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini, amesema “Huu ni mradi wa kihistoria, ambao unaondoa shida kubwa kwa wananchi, unapeleka huduma ya usafiri kuwa rahisi sana kwao… Bodaboda zitapita watu watapata ajira. Ni mradi ambao kwa kweli hata mimi mwenyewe ukikamilika, nitaona tumepiga hatua katika jimbo hili.”

Ameongeza “Makaravati yatajengwa kwa kiwango, mitaro itawekwa ili mvua ikinyesha maji yasiweze kuhamisha barabara na kuiharibu.

“Wataalamu ninawashukuru sana, muendelee kufanya kazi nzuri, niwatakie usimamizi mzuri wa huu mradi ukamilike kwa muda tuliokubaliana, ili wananchi wapate huduma.”


Naibu Waziri Waitara (kulia) na Mhandisi Marwa (kushoto) wakikagua barabara hiyo


Kwa mujibu wa Meneja wa TARURA Wilaya ya Tarime, Mhandisi Charles Marwa, thamani ya ufunguzi wa mradi wa wa barabara hiyo ni Sh milioni 712.954.

Mhandisi Marwa amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza Aprili na unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60, baada ya shughuli za kusafisha eneo la barabara, kung’oa mawe, kukata na kujaza udongo katika baadhi ya maeneo ya barabara.

Aidha, ametaja manufaa ya barabara hiyo kuwa ni pamoja na kuinua uchumi wa wananchi katika jimbo hilo, hususan wa kata za Kibasuka na Turwa, kurahisisha shughuli za ulinzi na usalama na kupunguza umbali kutoka kilomita 48 hadi 5.6 kwa wakazi wa maeneo ya Nyarwana na Tarime mjini kwa ujumla.




Awali, Naibu Waziri Waitara alitembelea shule za sekondari mbalimbali, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Manga jimboni hapo.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages