NEWS

Friday 24 September 2021

Waziri Mkuu Majaliwa amwagiza Waziri Gwajima kupeleka jokofu, daktari Ndungu Same




WAKATI Serikali ikijipanga kukamilisha ajira za watumishi sekta ya afya ili kuboresha huduma kwa wagonjwa nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Afya, Dkt Dorothy Gwajima kununua na kupeleka jokofu la kuhifadhi maiti na kuongeza daktari katika kituo cha afya Ndungu wilayani Same, Kilimanjaro.

Majaliwa ametoa agizo hilo alipokwenda kukagua ukarabati wa kituo hicho cha afya, kisha kuzungumza na wananchi katika eneo hilo.


Amesema Serikali imejipanga kujenga vituo vya afya viwili na hospitali mbili katika majimbo ya Same Magharibi na Same Mashariki ili kusogeza huduma za afya kwa jamii.

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amewapongeza madaktari wa kituo cha afya Ndungu kwa jitihada zao za kuwahudumia wagonjwa kituoni hapo.

Kwa upande wake, Waziri Gwajima amemwelekeza Katibu wa Wizara ya Afya, Dkt Makubi kupeleka daktari kwa ajili ya kusaidiana na aliyepo katika kituo hicho, kwani kimeonesha kuzidiwa na wagonjwa, ambapo kwa mwaka hufanya upasuaji kwa wagonjwa 305.


Waziri Gwajima akihutubia wananchi

Katika hatua nyingine, Dkt Gwajima amesema kuwa ili Tanzania iwe salama, wananchi wanatakiwa kushikamana kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, huku akiwahimiza kujitokeza kupata chanjo, kwani janga la UVIKO 19 bado lipo na linahatarisha maisha ya watu.

Katika hafla hiyo, Waziri Gwajima amesema Serikali imefanya ukarabati wa kituo cha afya Ndungu Same, kitengo cha maabara, chumba cha wazazi na cha kuhifadhi maiti, na kwamba tayari wizara imetenga shilingi milioni 35 kwa ajili ya kununua jokofu la vyumba sita, ambapo ameagiza MSD ihakikishe inapeleka jokofu kituoni hapo.



Akizungumzia mikakati ya kuboresha huduma za afya katika mkoa wa Kilimanjaro, Waziri Dkt Gwajima amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika hospitali ya mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi na kwamba ujenzi umefikia asilimia 70.

Awali, Mbunge wa Same Magharibi, Anne Kilango Malecela ameiomba Serikali kujenga hospitali mbili, kwani wilaya ya Same ina majimbo mawili yenye watu wengi, kiasi cha kusababisha msongamano mkubwa kwenye zahanati na vituo vya Afya.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Same)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages