NEWS

Saturday 25 September 2021

Vijana zaidi ya 1,000 wahitimu JKT Rwamkoma, Meja Jenerali Mabele awahimiza kuishi uaminifu, utiifu




WAHITIMU wa mafunzo ya mujibu wa sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini, wametakiwa kuwa chachu ya uaminifu, utiifu na uhodari wa kazi za maendeleo katika jamii.

Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajab Mabele ameyasema hayo jana Septemba 24, 2021, wakati akifunga mafunzo hayo kwa vijana 1,047 katika kambi ya Rwamkoma wilayani Butiama, Mara.

“Mmejifunza mbinu za kivita za kukabiliana na adui anayehatarisha uhuru, umoja na amani ya nchi, msizitumie mbinu hizi kuleta fujo mitaani na kuwa chanzo cha kuvunja amani katika jamii,” Meja Jenerali Mabele amewambia vijana hao, ambao pia ni wahitimu wa kidato cha sita mwaka huu.


Meja Jenerali Mabele akizungumza katika hafla hiyo.

Amewataka kwenda kutumia mafunzo hayo kuonesha uzalendo, kulinda nchi, kuishi na jamii kwa nidhamu, upendo, amani na umoja.

Aidha, Mkuu huyo wa JKT amewataka vijana hao kulinda afya zao, ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19) na Ukimwi, miongoni mwa maradhi mengine.

Kikundi cha vijana wa kike wahitimu wa mafunzo hayo kikipita kwa mwendo kasi mbele ya Meja Jenerali Mabele (hayupo pichani).

“Lindeni afya zenu, afya yako ni mtaji kwako, Taifa linawategemea sana,” amesema Meja Jenerali Mabele na kuwatakia masomo mema kwa watakaoendelea na masomo ya vyuo vikuu na vya kati.

Meja Jenerali Mabele (kushoto) akikagua ukakamavu wa wahitimu hao.

Awali, Kaimu Kamanda wa Kikosi cha 822 KJ Rwamkoma, Meja Kinana Memne amesema mafunzo hayo kwa vijana hao, yalianza Juni 21, mwaka huu.

Meja Memne amefafanua kuwa kati ya vijana 1,070 walioanza mafunzo hayo kambini hapo, waliohitimu ni 1,047 wakiwemo wa kiume 844 na wa kike 203. Wengine 23 hawakuhitimu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo utoro.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages