
Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara
Mara Online News
------------------------
Uchumi wa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) unaweza kukua kwa kasi wakati wowote kuanzia sasa, shukrani kwa ujio wa miradi ya kimkakati ambayo imeanza kutekelezwa kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.
Tayari mabiloni kadhaa ya shilingi yametemgwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo katika miji midogo ya Nyamongo na Nyamwaga.
Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa jengo la soko la dhahabu katika mji mdogo wa Nyamongo ulipo jirani na mgodi huo, ambao unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
“Tutajenga soko la dhahabu kubwa lenye ghorofa tatu na utekelezaji wa mradi huu umeishaanza,” Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa Barrick North Mara, Godfrey Kegoye, aliwaambia waandishi wa habari wilayani hapa wiki hii.
Alisema jengo hilo la soko la dhahabu litakuwa kitega uchumi kikubwa ambacho kitaiongezea pato Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.
“Kwa mchoro ambao tumeandaa tutakuwa na maduka na ofisi za kupangisha hata mabenki. Kitakuwa kitega uchumi kikubwa,” alisema Kegoye ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matongo.
Alitaja miradi mingine ya kimkakati itakayotekelezwa kwa kutumia fedha za CSR kuwa ni pamoja na ujenzi wa soko la kisasa na stendi katika mji mdogo wa Nyamwaga.
Miradi hiyo inatarajiwa kubadilisha muonekano wa maeneo hayo mawili na kuchangamsha shughuli za biashara.
Kegoye aliongeza kuwa utekelezaji wa miradi mingine ya CSR katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara inaendelea katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika Mgodi wa Barrick North Mara, Godfrey Kegoye.
Tatwimu zinaonesha kuwa mgodi wa Barrick North Mara umetoa shilingi bilioni 26 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2019 hadi 2025.
Wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo wanasema ujio wa miradi ya kimkakati ni neema ambayo itakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa wachimbaji wadogo wa madini, wafanyabiashara na wakulima.
“Ifahamike kuwa hapa Nyamongo kwa mfano, wananchi wengi wanajishughulisha na uchimbaji mdogo, hivyo uwepo wa soko la dhahabu jirani nao utakwa ni ahueni kubwa kwao,” anasema Felster Range, mkazi wa mji huo.
Felister ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, anasema mradi huo pia utakuwa mkombozi kwa wanawake na vijana wa maeneo hayo.
“Hata wanawake wengi hapa Nyamongo wanajishulisha na uchimbaji mdogo wa dhahabu, hivyo watanufaika pia,” anaongeza.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Nyamwaga, Ambroze Chacha Nyangoko, anasema ujenzi wa soko na stendi ya mabasi katika eneo hilo vitachochea ukuaji wa uchumi kwa wakulima na wafanyabishara wa bidhaa mbalimbali.
“Kwanza kwa sasa mabasi yanapita Nyamwaga bila kusimama kwa kuwa hakuna stendi ya mabasi, uwepo wa stendi utaongeza mapato. Ujenzi wa soko pia utachangamsha biashara hapa kwetu. Watu wataleta samaki kutoka Ziwa Victoria, na bidhaa zingine kama ndizi zitapata soko zaidi tofauti na ilivyo sasa,” anasema Nyangoko.
Wananchi hao walitoa wito kwa mamlaka husika kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo. “Mfano, ujenzi wa soko pia utatoa fursa za vibanda kwa wafanyabiashara wakiwemo vijana. Ningeshauri ujenzi wa hii miradi uanze haraka bila kuchelewa,” alisema mmoja wao.
Kwa mujibu Mkurengezi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Solomon Shati, maandalizi ya utekelezaji wa miradi yanaendelea vizuri.
No comments:
Post a Comment