NEWS

Sunday 19 September 2021

Waziri Gwajima ahimiza maadili ya wauguzi, wakunga




WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima (wa tatu kushoto waliokaa) amewakumbusha wauguzi na wakunga kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadini na miongozo ya taaluma zao, kinyume chake watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Dkt Gwajima ametoa agizo hilo wakati akizindua Baraza la Uuguzi na Ukunga nchini, katika hafla iliyofanyika Kibaha mkoani Pwani, Septemba 18, 2021.

“Wakunga na wauguzi mnaoongozwa na baraza hili, nawaomba sana kwamba msijenge utaratibu wa kukiuka maadili, miongozo na kanuni," amesema.


Waziri Gwajima (katikati)

Ametumia nafasi hiyo pia kulitaka baraza hilo kutowafumbia macho wauguzi na wakunga wanaokiuka sheria, maadili, miongozo na miiko ya taaluma zao.

"Baraza msisite kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu na sheria zinazowaongoza na msimuonee mtu,” Waziri Gwajima amesisitiza.

Amelitaka baraza hilo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na salama, ili kuondoa malalamiko katika jamii.


Waziri huyo amesisitiza kuwa Baraza hilo lina wajibu wa kulinda, kuimarisha na kuhifadhi afya ya jamii, usalama na ustawi kupitia usimamizi na udhibiti wa shughuli za mafunzo ya uuguzi na ukunga.

Aidha, amelitaka kutimiza majukumu yake kwa weledi bila ya hofu ya kuingiliwa katika maamuzi litakayofanya kwa lengo la kuboresha sekta ya afya, hususan kwenye eneo la uuguzi na ukunga nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya, Ziada Sellah amempongeza Waziri Gwajima kwa uteuzi makini wa Baraza hilo, linalotarajiwa kuwa chachu ya kuleta matokeo chanya katika usimamizi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi, kwa kufuata sheria na kanuni za uguzi na ukunga.

Amelipongeza Baraza lililomaliza muda wake kwa jitihada kubwa za kufanya maboresho, ikiwemo kuanzisha mfumo wa kanzidata ambao umewezesha kutoa huduma kwa njia ya mtandao, kupata idadi ya wauguzi na wakunga kirahisi na kuhakiki usajili wao na uhai wa leseni zao za kutoa huduma.


Hata hivyo, amelitaka Baraza jipya kushughulikia changamoto zake, ikiwemo rasilimali fedha, ili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi.

Naye Mwenyekiti mpya wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Profesa Lilian Mselle, ameahidi kutimiza majukumu yake kwa weledi na kusisitiza kuwa Baraza hilo litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kuikuza zaidi taaluma hiyo na kuzalisha wahitimu wanaokidhi vigezo vya taaluma hiyo.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Kibaha)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages