NEWS

Wednesday, 22 September 2021

Waziri Gwajima akabidhi magari ya kufuatilia shughuli za afya, usafi wa mazingira mikoani




UFANISI wa shughuli za afya na usafi wa mazingira unatarajiwa kuongezeka nchini, baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt Dorothy Gwajima (pichani juu) kukabidhi magari saba kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli hizo mikoani, katika hafla maalum iliyofanyika jijini Dodoma, leo Septemba 22, 2021.


Halmashauri mikoani zimeendelea kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwenye vituo 873 vya kutolea huduma za afya na jamii nchini kwa mwaka wa fedha 2020/21, kupitia programu hiyo.


Waziri Gwajima (katikati) akikabidhi funguo kwa mmoja wa madereva wa magari hayo.

“Kama sehemu ya utekelezaji wa shughuli za afya, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatekeleza programu ya huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira, yaani Sustainable Rural Water Supply and Sanitation Program, yenye lengo la uboreshaji na upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira vijijini.

“Program hii inatekelezwa kwenye mikoa kumi na saba katika halmashauri 86 nchini. Mikoa hiyo ni Kagera, Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Tabora, Katavi, Singida, Rukwa, Songwe, Iringa, Manyara, Ruvuma, Lindi na Mtwara,” Dkt Gwajima amesema.


Kwa mujibu wa Waziri Gwajima, programu hiyo itatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2019-2024), ikilenga kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira katika shule na vituo vya kutolea huduma za afya na jamii.

Inatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


“Wizara itaendelea kuwezesha halmashauri na mikoa kutatua changamoto za usafiri kwa kadri itakavyopata rasilimali fedha kupitia program hii na kutenga fedha za kununua vyombo vya usafiri, ambapo kwa mwaka huu wa fedha, wizara itanunua magari mengine matano kwa ajili ya mikoa.

“Serikali imenunua pikipiki 138 ambazo tayari zinatumiwa na maafisa afya ngazi ya kata, kama sehemu ya utatuzi wa changamoto ya usafiri,” Waziri Gwajima ameongeza.

(Na Mwandishi wa Mara Online News, Dodoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages