NEWS

Tuesday, 28 September 2021

Waziri Kabudi amuagiza DPP kusimamia kesi za mazingira




HUENDA uharibifu na uchafuzi wa mazingira ukapungua, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kumuagiza Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kusimamia kesi kubwa za mazingira, badala ya kuziacha kwa wanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Bodi za Mabonde pekee.

“Naomba DPP asimamie kesi kubwa za mazingira, wanasheria wa NEMC wanadhani DPP hayupo,” Waziri Kabudi ameagiza wakati akifungua jengo jipya la Ofisi ya Taifa ya Mashitaka Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wiki iliyopita.


Waziri Kabudi akizungumza katika hafla hiyo.

Jengo hilo limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 284 zilizotolewa na Shirika la Grumeti Fund.

Profesa Kabudi amesema NEMC imekasimiwa kusimamia sheria za mazingira, lakini Ofisi ya DPP ndiyo yenye dhamana ya kusimamimia sheria zote za kulinda rasilimali za nchi, ikiwemo utunzaji wa mazingira.

Amegusia pia taasisi za Serikali zinazosimia sheria za utunzaji wa mabonde, likiwemo Bonde la Ziwa Victoria kwamba nazo zimekasimiwa kusimamia sheria za kulinda mazingira.

“NEMC wajue DPP yupo na nitaongea na Waziri wa Mazingira. Kuharibu mazingira ni makosa ya jinai,” Waziri Kabudi amesisitiza.

Wizara inayoshughulikia masuala ya mazingira ipo katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na waziri wake wa sasa ni Selemani Jafo.


Waziri Kabudi (katikati waliokaa) na baadhi ya viongozi wa Serikali ngazi ya Taifa na mkoa wa Mara (waliokaa), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wazee maarufu wa wilayani Serengeti (waliosimama nyuma).

Waziri Kabudi amesema “Ujangili pia ni uhujumu uchumi. Jambo lingine ni ukataji wa misitu. Misitu inakatwa bila huruma. Kuharibu misitu ni kosa la jinai.”

Ametaja eneo jingine ambalo ofisi ya DPP inapaswa kumulika kwa makini kuwa ni sekta ya madini.

“Madini ni eneo ambalo linahitaji ukali. Linahusika katika utoroshaji wa madini na kulikosesha Taifa mapato,” Profesa Kabudi amesisitiza.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages