NEWS

Monday 25 October 2021

DC Machali ataka wanafunzi wacharazwe bakoraMKUU wa Wilaya (DC) ya Bukoba mkoani Kagera, Moses Machali (pichani juu aliyesimama kulia), ametaka walimu wasiogope kuchapa wanafunzi vibobo kama njia ya kuwasaidia kutimiza ndoto zao za kusonga mbele kielimu na kudhibiti nidhamu inayoporomoka.

Akizungumza na wanafunzi na walimu wa Shule ya Sekondari Nshambya katika Manispaa ya Bukoba, baada ya kupokea msaada wa viti na meza kutoka Benki ya NMB hivi karibuni, Machali amesema lazima wanafunzi wadhibitiwe kwa ‘bakora’, akisema baadhi ya viongozi wamepita katika mkondo huo.

Hata hivyo, Machali ambaye amewahi kuwa Mbunge, amewakumbusha walimu hao kutoa adhabu ya viboko kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa kuhusu utoaji wa adhabu kwa wanafunzi, ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.

Mwaka 2019, Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ilimtia hatiani mwalimu Respicius Mutazangira wa Shule ya Msingi Kibeta na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kumuua kwa kumpa adhabu mwanafunzi Sperius Eradius.

Katika hukumu hiyo, Jaji Lameck Mlacha pia alirejea sharia na waraka wa elimu, unaotoa maelekezo ya utoaji wa adhabu kwa mwanafunzi kuwa itumike fimbo nyepesi, izingatie umri, afya na viboko visizidi vinne ambavyo lazima viandikwe kwenye kitabu na mwalimu aliyetoa adhabu hiyo.

Pia, DC Machali amewataka wanafunzi hao kutotegemea mteremko kama wanataka mafanikio kielimu bila kuwa a nidhamu, kuzingatia maelekezo ya walimu na kuongeza bidii katika masomo.

Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus amesema wataendelea kurudisha sehemu ya faida ya biashara yao kwa wananchi na kuwataka wanafunzi kujiandaa kunufaika na fursa mbalimbali za kielimu zinazotolewa na benki hiyo.

Ladislaus amesema NMB imeanzisha utaratibu wa kufadhili masomo ya sekondari na vyuo vikuu kwa wanafunzi wenye ufaulu mzuri wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo - kupitia NMB Foundation, na kuwataka waongeze bidii waweze kufikia ndoto zao.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nshambya, Fredrick Bulija, amesema msaada huo wa viti na meza vyenye thamani ya Sh milioni 10, umepunguza changamoto ya wanafunzi kukosa sehemu ya kukaa na mazingira rafiki ya kutoa elimu.

Nayo Shule ya Msingi Nshambya imenufaika na mgao wa viti na meza 50, ambapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Jasson Gervase amesema msaada huo umemaliza tatizo lililokuwepo shuleni hapo.

(Habari na picha: Phinias Bashaya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages