NEWS

Wednesday, 7 January 2026

Naibu Waziri Kundo akagua utekelezaji wa miradi ya maji Serengeti, Bunda



Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew (aliyevaa suti na miwani), akikagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, mkoani Mara mapema wiki hii.

Na Mwandishi Wetu
Mara
---------

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amemtaka mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, mkoani Mara, kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati.

Naibu Waziri Kundo alitoa maelekezo hayo mapema wiki hii alipokwenda kukagua maendeleo ya utekelezaji mradi huo, ambapo alimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya kazi.

Alisema serikali haidaiwi na imekuwa ikitoa fedha za utekelezaji wa mradi huo kwa wakati kuuwezesha kukamilika kwa wakati na kuanza kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.

Mradi huo wenye thamani ya shilingi zaidi ya bilioni 21, unatekelezwa na Mega Engineering and Infrastructure Company Limited kutoka nchini India.

Naibu Waziri Kundo alimhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Wakili Angelina Lubella, kwamba Wizara ya Maji imejipanga kuhakikisha kuwa miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika wilaya hiyo inakamilika kwa wakati na kuboresha huduma ya maji kwa wananchi.

Mradi huo wa miji 28 ukikamilika unatarajiwa kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wakazi zaidi ya 100,000 wa mji wa Mugumu na vijiji jirani.

“Kila mmoja atimize wajibu wake, tunataka kuona maji yanatoka kwa ajili ya wananchi wa Serengeti, kwa sababu hatuna shida ya fedha katika huu mradi. Huu mradi fedha yake ipo - haina changamoto yoyote… kila hatua wanalipwa kulingana na ambavyo tumekubaliana,” alisema Naibu Waziri Kundo.

Hivyo, alimtaka mkandarasi kuacha uzembe aliouita wa kimataifa. “Mkandarasi sitaki kusikia tuko kwenye mchakato wa kuandaa mazingira ya kuchimba bomba lipite – sijui nini sitaki kusikia,” alisisitiza.

Lakini pia, Naibu Waziri huyo alimtaka mkandarasi kuhakikisha anaongeza idadi ya wafanyakazi wenye vigezo stahiki ambao watasukuma mradi huo ukamilike kwa wakati na kuanza kuhudumia wananchi.

“Waandae mazingira ya kufanya kazi usiku na mchana, lakini vilevile ndani ya wiki mbili kuanzia sasa, tunataka kuona subcontractor anapewa vifaa vyote vinavyohitajika ili kuhakikisha kwamba mradi huu unaendelea bila kusuasua,” alielekeza.

Kuhusu wafanyakazi wenye vigezo kukimbia kwa sababu ya kutolipwa mishahara, alimtaka mkandarasi sasa kuhakikisha anapeleka kwa Mkuu wa Wilaya na Wizara ya Maji orodha ya wafanyakazi waliopo na kiasi cha malipo yao kwa mwezi kwa ajili ya ushahidi wa makubaliano yao.

Naibu Waziri Kundo Mathew (aliyevaa miwani), akitoa maelekezo kwa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 katika mji wa Mugumu wilayani Serengeti, mkoani Mara alipokwenda kuukagua.

“Tujidhihirishe kwamba wafanyakazi wa mradi huu ni akina nani, Wana vigezo Fulani viliVYOtamkwa kwenye mkataba, lakini mishahara yao inaendana na maelekezo ya serikali na sheria ambazo zinaongoza wakandarasi.

“Kwa hiyo, tunaamini kwamba hizi changamoto ndogondogo kwa pamoja tukizifanyia kazi, mradi wetu utaenda kwa haraka,” alisema Naibu Waziri Kundo.

Kukamilika kwa mradi huo kutawezesha Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuboresha zaidi huduma ya maji katika mji wa Mugumu na maeneo jirani.

Mbali na kupunguza tatizo la uhaba wa maji, mradi huo unatarajiwa kuongeza shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kutumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji badala ya kutafuta maji.

Akiwa wilayani Bunda Naibu waziri wa maji muhandi Jundo Merthiwe alikagua Mradi wa Majisafi wa Butiama-Nyamswa ambapo alielezea kuridhika na kazi zinazoendelea, lakini akamtaka mkandarasi kuongeza kasi ili ifikapo Februari 2026 wananchi waweze kupata huduma hiyo.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi zaidi ya billion nane, unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 5,000 katika vijiji vya Ikizu na Nyamuswa.

Kisha Naibu Waziri Kundo alitembelea na kuweka jiwe la msingi Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Majisafi Migungani-Kaswaka na kukagua maendeleo ya Mradi wa Majisafi Nyamuswa.

Aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWUSA) kwa ubunifu wa kukabiliana na tatizo la upotevu wa maji katika mradi huo.

Inaelezwa kuwa BUWASA imekuwa ikipoteza shilingi zaidi ya milioni 600 kwa mwaka kutokana na ubovu wa mabomba ya mtandao wa mradi huo.

Mkurugenzi wa BUWASA, Easter Giriyoma, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaiwezesha mamlaka hiyo kuondokana na upotevu wa maji na kuiwezesha kuwa na huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kundo alizungumza na watumishi wa BUWASA na kuwasisitiza kuendelea kushirikiana na kujituma katika utekekezaji wa majukumu yao.

Alitumia nafasi hiyo pia kusisitiza matumizi ya teknolojia nchini, ikiwemo matumizi ya dira za malipo kabla kama ilivyoelekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages