NEWS

Wednesday 13 October 2021

Kafulila: Rais Samia ameonesha mfano wa kuigwa Afrika kuhusu matumizi ya fedha za IMF/UVIKO-19David Kafulila

Rais Samia na matumizi ya fedha za IMF, somo kwa Afrika

Imeandikwa na David Kafulila, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu

Oct 13, 2021

Kwanza, Kwa miongo kadhaa kumekuwa na mjadala kwamba Afrika haiwezi kuendelea kwa kutegemea misaada na zaidi utegemezi wa misaada umehusishwa na kuongezeka kwa umasikini wa bara la Afrika.

Nikumbushe alichoandika mchumi nguli, Dambisa Moyo kwenye kitabu chake DEAD-AID, amesisitiza hoja hiyo katika ukurasa wa 11, ambapo ameonesha kuwa wakati kiwango cha misaada kwa bara la Afrika kilikuwa juu zaidi (peak) katika miaka ya 1970s mpaka 1998, hicho ndio kipindi ambacho Afrika ilitoka kuwa na asilimia 11 ya masikini wote duniani mpaka asilimia 66.

Hata hivyo, wapinzani wa hoja kuwa misaada inaongeza umasikini wamejenga hoja yao katika misingi kuwa tatizo ni udhaifu wa Serikali za Afrika katika kupanga na kutekeleza matumizi ya fedha za misaada kutokana na rushwa, ufisadi, matumizi mabovu na zaidi kupangiwa matumizi na watoaji mikopo na misaada.

Zaidi, wapinzani wa hoja kwamba misaada ni sababu ya umasikini wanasisitiza hoja yao kwa kurejea mfano wa namna msaada wa Marekani chini ya mpango wake wa 'Marshal plan' wa $15bn ulivyofufua uchumi wa Ulaya baada ya Vita ya II ya Dunia na kuhoji kwanini Afrika inayopokea misaada takribani $50bn kwa mwaka, bado imezidi kuwa bara linalozidi kudidimia kwenye umasikini.

Kwamba Afrika kutoka kuwa bara lenya asilimia 11 ya masikini wote duniani mwaka 1970s mpaka asilimia zaidi ya 70 ya masikini mwaka 2019, na inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030, Afrika litakuwa bara lenye asilimia 87 ya masikini wote duniani. (Ripoti ya Taasisi ya Utafiti BROOKINGS, March28, 2019).

Ni hoja yangu kwamba kilichotokea kwenye msaada/mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa UVIKO-19 kwa nchi za Afrika, kinathibitisha hoja ya kwanini tatizo sio misaada bali wanaopewa misaada.

Kwamba, wakati mataifa mengi barani Afrika yametumia sehemu kubwa ya fedha za IMF za kupambana na UVIKO-19 kwa semina, warsha, kampeni, ununuzi wa vifaa tiba kukabili ugonjwa huo kwenye hospitali na vituo vya afya, makongamano ya uelimishaji na ununuzi wa shehena za barakoa kujikinga na ugonjwa huu, Rais wetu Samia Suluhu Hassan (SSH) amefanya tofauti kwa lengo lile lile.

Ndio msingi wa hoja kwamba Rais SSH amejenga hoja IMF na kukubalika kwamba kukabili UVIKO-19 Tanzania inahitaji kuongeza madawati na madarasa ili wanafunzi wasibanane darasani na hivyo kupunguza uwezekano wa wanafunzi kuambukizana ugonjwa huo.

Kwa sababu hii, Rais SSH amefuta tatizo la madawati na madarasa kwa mwaka 2022 kwa kutenga sehemu ya fedha za IMF/ UVIKO-19 kukamilisha maboma ya madarasa 15,000 na madawati 462,795. Nguvu na muda ambao ungetumika kulitatua tatizo hili tutavitumia kushughulika na changamoto nyingine.

Kwamba yanunuliwe magari 25 ya kuchimba visima kila mkoa na mitambo mitano ya kuchimba mabwawa ili kupunguza tatizo la upatikanaji maji kama njia ya kukabili UVIKO-19.

Nakumbuka Ripoti ya Taasisi ya Tafiti za Maoni (Opinion Survey) ya SYNOVATE ambayo ni ya tano kwa ukubwa duniani, mwaka 2008 ilionesha kuwa maji ndio ilikuwa kero namba moja Tanzania.

Maji ni uhai, na tafiti zinaonesha kwamba kwenye kila $1 inayowekezwa kwenye mradi wa maji inaokoa $4.2 ambazo zingetumika kutibu magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama (WHO Report, Nov 19, 2014).

Hivyo Rais SSH anazitumia fedha za IMF/ UVIKO-19 kukabili tatizo la maji ambalo ni ajenda ya nchi hata kabla ya UVIKO-19. Amelitumia tatizo la UVIKO-19 kukabili tatizo la upungufu wa magari ya kubeba wagonjwa kwa kununua magari 395 yatakayosambazwa vituo vya afya na hospitali nchi nzima.

Na kwamba tuongeze vyuo vya VETA 32 ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kuepuka kuambukizana UVIKO19. Yote hii ni Rais SSH anatekeleza ajenda ya Dira ya Taifa ya 2025 ya kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi kiasi (semi-skillied) kwa kutumia fedha za IMF/UVIKO-19.

Ni wazi kama bara la Afrika lingekuwa na viongozi wenye fikra kama za Rais wetu SSH kuhusu matumizi ya mikopo nafuu na misaada, wana wa Afrika wangeona tofauti kubwa sana kwenye mataifa yao.

Ukisoma taarifa ya IMF ya Oktoba 08, 2021, kiasi cha $26.46bn au zaidi ya TZS 60.86/trilioni kilichokwishatolewa kwa ajili ya kukabili UVIKO-19 kwenye nchi za Afrika - Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambao ni ukanda masikini zaidi duniani kwa kwa ajili ya mpango wa kukabili UVIKO-19, ni wazi kama nchi hizo zingekuwa na mfumo kama wa Tanzania chini ya Rais SSH, zingeacha alama kubwa sana ya maendeleo.

Lakini ndio hivyo, wengi zimeishia kuagiza barakoa na vifaa vya hospitali, semina, warsha na makongamano ya kujengeana uwezo wa namna ya kujikinga na UVIKO 19.

Wakati Tanzania imepata $567m na Rais anakuja na mpango ambao sio tu wenye uwazi na tija kubwa kwenye uchumi wa nchi, bali kwa uwazi wa kiwango cha juu hata kufanya Watanzania kuona fahari ya mkopo husika.

Leo sitaki kuongelea kinachoendelea kwa jirani rafiki na jirani utaratibu wa fedha hizo za IMF/ UVIKO. Hadi siku nyingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages