NEWS

Monday 4 October 2021

Maendeleo Musoma Vijijini: Gomora wajenga shule kuondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefuWAKAZI wa kitongoji cha Gomora kilichopo kijiji na kata ya Musanja katika Jimbo la Musoma Vijijini, wameanza ujenzi wa shule mpya ya msingi kuondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda masomoni.

Kwa mujibu wa Msaidizi wa Mbunge wa Jimbo hilo, Verediana Mgoma, ujenzi huo umeanza hivi karibuni.

Mgoma amesema kwa sasa wanafunzi kutoka kitongoji hicho wanalazimika kutembea umbali wa kilomita nne kwenda kusoma katika Shule ya Msingi Musanja iliyoanza mwaka 1956 kijijini hapo.

“Wengine wanalazimika kutembea umbali mrefu zaidi kwenda kusoma katika shule za msingi Lyasembe (iliyopo kata ya Murangi) na Bwenda (katani Rusoli),” Mgoma ameongeza.

Kata ya Musanja inaundwa na vijiji vitatu, ambavyo ni Musanja, Nyabaengere na Mabui Merafuru.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Musanja, Ngasa Msabi amesema shule hiyo ina wanafunzi 815 wa darasa la kwanza hadi la saba, vyumba saba vya madarasa, walimu wanane, upungufu wa vyumba 12 na walimu 10.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Gomora, Sospeter Mjarifu amesema wakazi wa kitongoji hicho wameamua kujenga shule yao kutokana na michango ya wanakijiji, Diwani wa Musanja, Mbunge wa Musoma Vijijini na wadau wengine wa maendeleo.

Mjarifu amesema hadi sasa wanakijiji wameshachimba msingi wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu, kusomba mawe, mchanga, maji na kila kaya kuchangia shilingi 15,000.

Aidha, Diwani wa Kata ya Musanja, Ernest Mwira ameitisha harambee ambayo yeye na wadau wa maendeleo wamefanikisha michango ya fedha taslimu shilingi milioni 1.3, saruji mifuko 63 na nondo nane.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Profesa Sospeter Muhongo ameanza kuchangia ujenzi huo saruji mifuko 50.

“Lengo kuu la wanakijiji ni kuona shule shikizi ya Gomora inafunguliwa Januari 2022,” amesema Mgoma.

Ameongeza “Ombi kutoka kitongoji cha Gomora ni kupata michango kutoka Halmashauri yetu na kwa wadau wengine wa maendeleo ili kukamilisha ujenzi wa shule shikizi ya Gomora.”

Kwa mujibu wa Katibu huyo wa Mbunge, wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini kwa sasa wanajenga shule za msingi mpya (shule shikizi) 12, ili kuondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda masomoni na mirundikano madarasani.

Mgoma amezitaja shule hizo kuwa ni Binyago, Buanga, Buraga, Egenge, Gomora, Kaguru, Karusenyi, Kihunda, Mwikoko, Nyasaenge, Rwanga na Ziwa.

Amebainisha kuwa kwa sasa shule za msingi zilizopo Musoma Vijijini ni 111 za Serikali na tatu za binafsi.

(Na Mwandishi wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages