NEWS

Saturday 2 October 2021

Watumishi Tarime Mji wazindua mazoezi ya viungo
MKUU wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele amezindua rasmi mazoezi ya viungo kwa watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, yatakayokuwa yakifanyika kila Jumamosi.

Akizindua mazoezi hayo leo Septemba 2, 2021 katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime, Kanali Mntenjele amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kujitokeza kila mara kwenye mazoezi hayo, kwani yanasaidia kujenga ukakamavu na kuimarisha afya ya mwili.


Kanali Mntenjele (wa tatu kulia) akikagua timu ya soka

Pia, Kanali Mntenjele amewataka walaamu wa afya kuhudhuria vipindi vya mazoezi hayo, ili kuwapima afya washiriki na kutoa ushauri wa kitaalamu.

“Lazima utujue umhimu wa mazoezi kwa afya zetu sisi ambao ni watumishi. Nitoe wito tunapokuwa na mazoezi kama haya wataalamu wa afya wawepo kwa ajili ya kupima washiriki kwa magonjwa ambayo vipimo vyake sio gharama kubwa ili wajue afya zao,” Kanali Mntenjele amesema.Aidha, Kanali Mntenjele amewataka walimu wanaosoma michezo chuoni hapo kupenda taaluma hiyo, ili wakihitimu waitumie kuhamasisha mazoezi na michezo shuleni.

Naye Afisa Michezo Wilaya ya Tarime, Teddy Musyangi ambaye ameratibu mazoezi hayo, amesema uzinduzi huo umefanyika sambamba na michezo ya soka, pete na kufukuza kuku kati ya timu za Halmashauri ya Mji wa Tarime na Chuo cha Ualimu Tarime.


Teddy Musyangi akimiliki mpira wa pete uwanjani

“Mazoezi haya ya viungo yatakuwa yakiendelea katika viwanja hivi kila Jumamosi asubuhi, tunawakaribisha watumishi wote kuhudhuria, kwa ajili ya kujenga afya zao, na hata wadau wengine wa michezo wakijisikia, tunawakaribisha waje tuungane hapa,” Teddy amesema.

(Habari na picha: Mobini Sarya)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages