
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
------------

Mwanza
------------
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane imeandika historia mpya katika sekta ya uhifadhi na utalii Tanzania, baada ya kuadhimisha ‘Birth Day’ ya Miaka 10 ya Simba inaowahifadhi.
Sherehe hiyo iliyobeba kaulimbiu inayosema “Saanane King Turns 10” ilifanyika Jumamosi, Desemba 20, 2025 ikilenga kuongeza hamasa na kukuza utalii kwenye hifadhi hiyo iliyopo katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza.

Birth Day hiyo ya Mfalme wa Pori, ilihusisha matukio ya watalii kuwaona mbashara (live) simba wakilishwa keki maalum, pamoja na kupata simulizi kuhusu tabia, maisha na umuhimu wa wanyamapori hao katika uhifadhi na utalii.
Aidha, tukio hilo la kipekee, liliandaliwa ili kuenzi umaarufu wa simba ambao licha ya kuwa na sifa za ukali, jasiri na mahiri katika kuwinda, wameendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo muhimu cha mapato kwa taifa kupitia sekta ya utalii.
Akizungumza katika sherehe hiyo, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Msimamizi wa Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Cesilia Nkwabi, alisema simba wana umuhimu mkubwa katika uhifadhi na utalii.

Simba wa Kisiwa cha Saanane
“Simba ni miongoni mwa wanyamapori watano wakubwa (big five), ni kivutio kikubwa cha utalii na ni sehemu ya wanyama wanao- balance (sawazisha) mwingiliano wa kiikolojia kwenye maeneo yanayohifadhiwa.
“Kwa hiyo, kupitia tukio hili la kuadhimisha Birth Day ya Simba wa Kisiwa cha Saanane, tunaendelea kuhimiza uhifadhi wa wanyamapori na mazingira wanayoishi ili waendelee kuwepo vizazi hata vizazi,” alisema Cesilia.

Cesilia Nkwabi
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Himasheria na Ulinzi Mkakati, Pellagy Marandu, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Tutindaga George, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa hifadhi hiyo na TANAPA kwa ujumla.
“Tunaadhimisha birth day hii ili pia kuendelea kumtangaza simba katika hifadhi hii ya kipekee, tuendelee kumuenzi na kumthamini,” alisema.

Pellagy Marandu,
Watalii wa ndani, wakiwemo wanafunzi walipata fursa ya kuuliza na kujibu maswali kuhusu uhifadhi wa simba na wanyamapori wengine, ambapo washindi walipewa zawadi kemkem, ikiwemo mabegi yenye picha ya simba na nembo ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.
Mwongoza Wageni wa hifadhi hiyo, Sanura Heri, aliwaelimisha watalii hao kuhusu tabia, makazi na umuhimu wa simba katika mfumo wa ikolojia ya maeneo yanayohifadhiwa.

Baadhi ya watalii hao, wakiwemo Japhet Boaz na Debora Japhet, waliipongeza Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane kwa ubunifu wa kuandaa tukio hilo la kihistoria, na wakatoa wito wa kuwahimiza Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa ili kujifunza na kufurahia vivutio vya wanyamapori na mazingira.
Wanafunzi wa Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, wakiwemo Naishon Ngarash Mollel, Safiel Elietiniswi Mnzava, Junior Mzamin Magwali na Ester Anjelo George, walisema tukio hilo limewapa uelewa mpana kuhusu maisha ya simba.
Walisema wengi wao hawakuwa wanajua kuwa simba anayehifadhiwa ndani ya uzio anaweza kuishi hadi miaka 20, tofauti na anayekuwa huru porini.

Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ikiwa na hadhi ya kipekee kama hifadhi ya kwanza nchini iliyopo katikati ya mji.
Hifadhi hii iko umbali wa kusafiri dakika 10 tu kwa usafiri wa boti kutoka katikati ya jiji la Mwanza, jambo linaloifanya kuwa kivutio rahisi kufikika kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mbali na simba (Mfalme wa Pori), Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ina vivutio vingi vya utalii, ikiwa ni pamoja na wanyamapori wengine kama vile swala, pundamilia, nyumbu, pimbi, tumbili, digidigi, fisi maji na mamba.
Pia, hifadhi hii ina huduma za boat safari katika Ziwa Victoria, rock hiking, maeneo ya mapumziko (picnic sites), michezo majini, kutazama machweo ya jua na malazi ya kitalii.


No comments:
Post a Comment