NEWS

Wednesday 3 November 2021

Grumeti Fund yawezesha maelfu ya wasichana kufikia ndoto zao za elimu


MPANGO wa kuwezesha wanafunzi wa kike wa shule za sekondari kupata elimu bila vikwazo, umewaweka maelfu ya wasichana kwenye nafasi nzuri ya kufikia ndoto zao za elimu katika wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara.

Mpango huo ulianzishwa na Shirika la Grumeti Fund mwaka 2018, baada ya utafiti wao kubaini vikwazo kadhaa vilivyokuwa vinakatisha ndoto za elimu kwa watoto wa kike.

Vikwazo hivyo ni mila kandamizi, kama vile ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni. Kikwazo kingine kilikuwa ukosefu wa taulo za kike, hali iliyosababisha wengi wao kutohudhuria shule wanapokuwa kwenye hedhi.Jambo la kufurahisha ni kwamba shirika hilo ambalo linasaidia uhifadhi kwenye mapori ya akiba ya Ikorongo/Grumeti na maendeleo ya jamii katika vijiji 22 vilivyo jirani na mapori hayo, limeweza kupunguza matatizo hayo kwa kuwezesha wanafunzi wa kike 6,000 kutambua thamani yao na umuhimu wa elimu.

Utekelezaji wa mpango huo umeshuhudia uwepo wa matamasha ya kuwezesha wasichana kutoka shule mbalimbali katika wilaya hizo kupata mafunzo ya kuwezesha na kuhamasisha wasichana kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao.

Mfano mwaka huu, mpango huo umefanikiwa kufikia wasichana 2,391 na wavulana 632.

“Tunafuraha kuwa kwa mwaka huu [2021] tu, tumeweza kufikia kufikia wasichana 2,391 na wavulana 632 kutoka shule 12. Lengo la matamasha hayo ni kuwezesha na kuhamasisha wasichana kufikia ndoto zao za elimu ,” Meneja wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Grumeti Fund, Frida Mollel ameiambia Mara Online News wilayani Serengeti, hivi karibuni.Frida amesema matamasha hayo yalifanyika kati ya Mei na Oktoba mwaka huu, huku kwa mara ya kwanza mpango huo ukipiga hatua zaidi kwa kuhusisha wavulana ili waweze kuwa sehemu ya mafanikio ya wasichana kufikia ndoto zao.

“Tumeona ni busara kuhusisha watoto wa kiume kwa sababu ni sehemu ya jamii, ili nao waweze kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za mabinti,” Frida amesema wakati wa ufungaji wa tamasha la wavuluna katika Shule ya Sekondari ya Issenye wilayani Serengeti, hivi karibuni.


Frida akihamasisha jambo katika tamasha la wavulana hao

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Chris Mauki amewataka wavulana hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii zao kuachana na dhana zinazomnyima mtoto wa kike fursa ya kupata elimu na maendeleo ya kiuchumi.

Dkt Mauki ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, amesema kuwezesha mtoto wa kike sio jukumu la Serikali na taasisi za kihisani pekee, bali ni la kila mtu katika jamii.

“Kila mtu anapaswa kumjali, kumpenda, kumheshimu na kumtetea mtoto wa kike,” amesisitiza.


Dkt Chris akizungumza na wavulana hao

Kwa mujibu wa Frida, shule za sekondari zilizofikiwa katika awamu ya kwanza Mei mwaka huu, ni Serengeti, Issenye, Makundusi, Nagusi, Rigicha na Nyichoka (Serengeti) na Hunyari na Chamriho (Bunda).

Awamu ya pili imehusisha wavulana kutoka shule za sekondari za Issenye, Rigicha na Nagusi, huku tamasha jingine lililofanyika hivi karibuni likihusisha wasichana 1,100 kutoka shule za sekondari za Mugumu, Manchira, Ikoma na Sedeko.Akigawa taulo za kike kwa wasichana hao 1,100 katika tamasha lililofanyika Shule ya Sekondari Mugumu, Frida amesema taulo hizo zinafuliwa na kuendelea kutumika katika kipindi cha mwaka mzima.

“Hizi taulo zinatumika kwa mwaka mzima na kama Grumeti Fund tumefurahi kuja na suluhisho la changamoto ya hedhi ambayo imekuwa ikisababishia wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria vipindi shuleni wakati wakiwa kwenye hedhi,” amesema.Frida akionesha taulo za kike alizogawa kwa wasichana hao

Wanafunzi hao wamepata mafunzo na uelewa zaidi kuhusu madhara ya mila mbaya ambazo zinaweza kukatisha ndoto zao za elimu, kama vile ukeketaji.

Mwanaharakati maarufu wa kupinga vitendo vya ukeketaji mkoani Mara, Rhobi Samwelly ambaye alikuwa mtoa mada ya masuala ya ukeketaji katika tamasha hilo amewataka wanafunzi hao kuwa mstari wa mbele kupinga mila hiyo katika jamii zao.

“Maisha ni elimu, kusoma na sio kukeketwa,” Rhobi amewambia wanafunzi hao.

Amesema ukeketaji ni moja ya vikwazo vinavyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike katika mkoa wa Mara.


Rhobi akitoa mada katika tamasha hilo

“Ukeketaji ni mila ambayo imepitwa na wakati. Mimi mwenyewe nilikeketwa na baada ya kupitia magumu sipendi kuona watoto wa kike wanakeketwa,” Rhobi ambaye pia ni mwanzilishi na mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT), amesema.

Mgeni rasmi katika tamasha hilo lililofanyika Shule ya Sekondari Mugumu, alikuwa Rhonda Vetere kutoka Marekani, ambaye ni mmoja wa wanawake 10 mabingwa wa teknolojia duniani.

“Someni kwa bidii ili muweze kutimiza ndoto zenu na msiruhusu mtu yeyote kuzima ndoto zenu,” Rhonda amewahimiza wanafunzi hao.


Rhonda (kulia) akizungumza na wasichana hao

Rhonda pia amepata fursa ya kuzungumza na kufurahia kucheza muziki na wanafunzi hao, huku kila mmoja akifurahia siku hiyo iliyojaa mafunzo, michezo na muziki.

Wanafunzi walioshiriki matamasha hayo wamelishukuru Shirika la Grumeti Fund, wakisema mafunzo waliyopata yamewajengea ujasiri wa kutetea haki zao na kusoma kwa bidii, ili hatimaye waweze kutimiza ndoto zao za elimu na uhuru wa kiuchumi.

“Ninawashukuru Grumeti Fund kutujengea uwezo wa kufikia ndoto zetu. Wametuelimisha madhara ya ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni na namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

“Lakini pia, hizi taulo za kike walizotugawia zimetuongezea hamasa ya kuhudhuria masomo shuleni bila kukosa hata wakati wa hedhi,” Faraja Sospeter (17) wa kidato cha nne kutoka Sekondari ya Nyichoka amesema.

Jane Amos (16) wa kidato cha tatu kutoka Sekondari ya Makundusi amesema mafunzo hayo yamemjengea uwezo wa kukabiliana na kushinda vikwazo vya elimu, ukiwemo ukeketaji.“Mafunzo haya yamenibadilisha, yana faida kubwa kwangu. Hata hizi taulo za kike zitatusaidia sana kujisitiri, na wametufundisha namna nzuri ya kuchoma zilizoisha muda wa kutumika, badala ya kuzitupa ovyo,” Jane amesema.

Damali Misolo (17) wa kidato cha nne kutoka Sekondari ya Serengeti, ameishukuru Grumeti Fund akisema “Nimenufaika na elimu ya afya ya uzazi waliyotupatia, wametujengea uwezo wa kujiamini na kushinda vikwazo. Natamani nikimaliza masomo na mimi niwe mhamasishaji wa mambo tuliyofundishwa.”

Naye mwanafunzi wa kiume, Magori Stephano wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Nagusi amesema “Mafunzo haya yameniwezesha kujua kwamba watoto wote; wa kike na wa kiume wana haki sawa, wote wanastahili kupata elimu na matunzo. Hata kazi za nyumbani tunapaswa kusaidiana.”

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages