Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo
WANANCHI katika Jimbo la Musoma Vijijini wameanza ujenzi wa shule za sekondari za kidato cha tano na sita za masomo ya sayansi (PCM & PCB).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Mbunge wa Jimbo hilo, tayari ujenzi huo umeanza katika Kata ya Kiriba.
Taarifa hiyo imesema wananchi wameonesha utayari wa kuchangia ujenzi wa miundombinu hitajika shuleni hapo.
“Maabara tatu za Fizikia, Kemia na Biolojia na jengo la utawala tayari yamekamilika na yanatumika. Pia ujenzi wa mabweni umeanza, utafuatiwa na ujenzi wa bwalo la chakula na jiko,” imesema taarifa hiyo.
Jimbo la Musoma Vijijini lenye kata 22 zenye vijiji 68, linaongozwa na Profesa Sospeter Muhongo.
Hadi sasa jimbo hilo lina shule za sekondari 22 ikiwemo moja ya kidato cha tano na sita za Serikali na mbili za binafsi, huku sekondari mpya 10 zikiendelea kujengwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, sekondari zote 22 na mpya zinajenga na kuboresha maabara za Fizikia, Kemia na Biolojia.
Shule za msingi zilizopo Musoma Vijijini ni 111 za Serikali na tatu za watu binafsi, huku shule mpya za msingi zinazojengwa zikiwa 13.
“Wadau kutoka ndani na nje ya Musoma Vijijini mnakaribishwa kuchangia ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu jimboni,” Mbunge Muhongo amesema.
(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)
No comments:
Post a Comment