
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba.
Tarime
-------------
Kijiji cha Matongo wilayani Tarime kinaendelea kushuhudia utekelezaji wa miradi mipya ya maendeleo kutokana na fedha zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Akizungumza na Sauti ya Mara hivi karibuni, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Charles Ryoba, alisema miradi inayotekelezwa kwa sasa imejikita katika kuboresha sekta ya elimu na miundombinu ya usafiri.
“Kwa sasa tunatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya shule na barabara kutokana na fedha za CSR kutoka Mgodi wa Barrick North Mara,” alisema Ryoba.
Alifafanua kuwa miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Matongo na nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Matongo.

Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari Matongo unaelekea kukamilishwa
Kwa mujibu wa Mwenyekiti Ryoba, ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa umetengewa shilingi milioni 64, jengo la utawala shilingi milioni 172, huku nyumba ya Mwalimu Mkuu ikigharimu shilingi milioni 85.
“Fedha zote hizo zimetolewa na mgodi kupitia mpango wa CSR, jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa kijiji chetu,” alisisitiza.

Ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Matongo unaendelea

Sehemu ya mbele ya jengo la nyumba ya Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi Matongo
Aidha, Ryoba alisema wana mpango wa kutekeleza mradi wa uzibuaji wa barabara yenye urefu wa kilomita 2.2, ambao utaboresha usafiri na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa kijiji hicho.
Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
Mpaka sasa, mgodi huo umetumia shilingi bilioni 26.86 kugharimia utekelezaji wa miradi ya CSR 255 katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ya msingi na sekondari, afya, barabara, maji, miradi ya kiuchumi na mazingira - tangu mwaka 2019 ulipokabidhiwa kwa Kampuni ya Barrick.
Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
No comments:
Post a Comment