NEWS

Tuesday 30 November 2021

Mataifa manne kupamba maonesho ya kilimo mseto Tanzania


WAWAKILISHI wa Shirika la VI-Agroforestry kutoka mataifa manne ya Afrika Mashariki wanatarajiwa kushiriki Maonesho ya Sita ya Kilimo Mseto, yaliyoandaliwa na shirika hilo la kimataifa katika mji wa Musoma nchini Tanzania.

“Maandalizi yote yamekamilika tayari kwa maonesho kuanza kesho. Tutakuwa na wawakilishi, yaani country representatives wa shirika la VI-Agroforestry kutoka Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania,” Afisa Miradi wa IDS, Davis Dominic ameiambia Mara Online News, mapema leo Desemba 1, 2021.

Tayari mashirika takriban 30 kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania, ikiwemo Dar es salaam, Dodoma, Kagera, Mbeya, Mwanza na Mara, yamethibitisha kushiriki maonesho hayo, yatakayofanyika kwa siku tatu mfululizo.

Kwa mujibu wa waandaaji, maonesho hayo yatafanyika katika kituo cha Mafunzo ya Kilimo Mseto (ATC) kilichopo Bweri, Manispaa ya Musoma mkoani Mara.Mwenyeji wa maonesho hayo ni Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, kupitia shirika lake la Maendeleo la Inland Development Services (IDS).

VI-Agroforestry ni shirika la kimaendeleo lenye makao makuu nchini Sweden, huku likielekeza nguvu kubwa katika kupambana na umaskini na mabadiliko ya tabianchi.

Mgeni rasmi katika maonesho hayo anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo.Kaulimbiu ya maonesho hayo mwaka huu inasema “Kilimo Mseto kwa Uhifadhi wa Mazingira na Kipato”.

Lengo kuu la maonesho hayo ni kueneza ujumbe kuhusu mchango wa kilimo mseto katika kuboresha hali ya maisha ya watu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

(Imeandikwa na Mara Onine News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages